May 15, 2022

Malima awaonya walimu wanaojihamisha kuholela Tanga


 Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima akizungumza na wananchi wa Kata ya Kibirashi wilayani Mkinga mkoani humo waliomsimamisha wakati wa ziara yake ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali wulayani humo, kujibu kero zao ikiwamo upungufu wa walimu.


Na Mwandishi Wetu

SERIKALI mkoani Tanga imebaini mtandao wa walimu ambao wamekuwa wakijiandikia barua feki ili kujihamisha shule katika Wilaya za Lushoto, Kilindi na Bumbuli.
 
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima amesema hayo jana wakati akijibu kero za baadhi wananchi waliomsimamisha akiwa ziarani wilayani humo kutembelea na kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa, kuhusu upungufu wa walimu katika kata ya Kibirashi na wilaya hiyo kwa ujumla ambapo ameonya kuhusu hatua hiyo.
 
Akizungumzia suala hilo, Malima alisema kulikuwa na tabia hiyo maeneo hayo matatu ya watu kuhama hama ambapo utakuta walimu wanakuja muda mfupi na kuhama na kuongeza kuwa hatua hiyo pia hufanywa na sekta ya afya.
 
“Sasa tumebaini kulikuwa na uhamaji kiholela baina ya Kilindi, Lushoto na Bumbuli ambapo walitengeneza kamtandao fulani wakawa wanajihamisha wenyewe kienyeji kwa barua feki. Lakini kuna hizo halmashauri tatu katika Mkoa wa Tanga ambazo zinaonewa kwa sababu wenyewe wanaona kama huku ni mbali na mazingira ya kufundishia wanaona ni magumu.
 
“Sasa jana (juzi) tulikuwa tulikuwa na Waziri wa Tamisemi (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa) tukasema tunataka tuangalie upya hii ikama, kwa sababu kimsingi hakuna sehemu ya Tanzania ambapo watoto wana haki pungufu ya kusoma. Yaani sisi kama serikali hatuangalii huku mjini basi kuwe na walimu wengi sasa wale watoto wa shamba wasipopata walimu watasoma vipi.
 
“Kwa hiyo elimu ya kila mtoto wa Tanzania ana haki sawa ya kupata elimu kutoka kwenye serikali yake. Kwa hiyo sisi hapa Tanga tumeamua walimu wanakwenda Kilindi, Lushoto na Bumbuli, vinginevyo walimu hao wanataka wahamie mjini basi wabebe na watoto wote wa Kilindi waende nao mjini wakawasomeshee kule,” alisema Malima.
 
Kwa upande wa walimu ambao hawataki kufundisha Kilindi, alisema wasije Mkoa wa Tanga wakatafute mikoa mingine ambayo kuna ubaguzi wa kupeleka kwenye maeneo lakini tabia ya kuona Tanga walimu wengi, Korogwe wengi huku Kilindi na Lushoto hakuna wanaona kubaya wanawanyima haki ya kusoma watoto wa maeneo hayo.
 
“Sasa hayo si maelekezo yangu, ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwamba wajukuu wake wote hawa wana haki sawa ya kusoma ndani ya Tanzania. Kwa hiyo mimi nakuombeni wazazi na walezi pale ambapo mnaona kwamba mnawapeleka watoto wenu shule lakini yule mtoto akirudi nyumbani ukimwangalia tu unasema wewe ulienda kucheza hukwenda kusoma ujue kuna tatizo na msilifumbie macho.
 
“Kwa maelekezo ya Rais katika sekta ya elimu na afya yako wazi, kila mtoto ana haki ya kusoma kwa hiyo sasa hapa ikionekana kuna walimu ambao hawatutendei haki au wametengeneza mfumo walimu wote wako Songe Kibirashi hakuna, mniambie mimi nitapata hizo taarifa na nitazifanyia kazi,” alisema.
 
Pamoja na mambo mengine, Malima alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Habel Busalama kumpa mgawo wa walimu kwa kila maeneo ya Kilindi ili aone wapi walimu wengi na wapi wachache kisha iangaliwe namna ya kufanya.
 
Kwa upande wake Ofisa Eilimu, Vifaa na Takwimu Sekondari wa Wilaya ya Kilindi, Noel Kombo alisema kwa ujumla Kata ya Kibirashi kama ilivyo kwa kata nyingine katika Wilaya ya Kilindi inakabiliwa na ikama ndogo ya walimu kulingana na idadi kubwa ya wanafunzi  kwa shule za msingi na sekondari.
 
Alisema wanafunzi ni wengi lakini ikama ya walimu wanayoletewa na Serikali Kuu bado haitoshelezi mahitaji ambapo hata hivyo jitihada zinaendelea kusawazisha ikama kwa fedha zinazoletwa na serikali hasa kwenye maeneo ambayo yana walimu wengi kuwasogeza katika maeneo ambayo yana uhitaji mkubwa.
 
“Hili tumekuwa tukiendelea nalo hasa kwa upande wa shule za sekondari ambapo hivi karibuni tumehamisha namba ya walimu karibu 15 kwenye sehemu yenye afadhali tumewapeleka maeneoa mbayo kuna uhitaji mkubwa, pia katika shule za msingi tunafanya hivyo.
 
“Hata hivyo hivi karibuni tumemaliza ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule shikizi kuna shule ambazo zina upungufu kwa hiyo juhudi zimekuwa zikiendelea kupitia kwa Mkurugenzi kuwasiliana na Tamisemi ili tuweze kuongezewa walimu,” alisema.
 

No comments:

Post a Comment

Pages