May 22, 2022

Mkurugenzi Bandari ya Dar es Salaam awaondoa shaka wafanyabiashara ucheleweshaji utoaji mizigo

 
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Juma Javara akijibu maswali yaliyoulizwa na Wafanyabiashara katika Kikao cha Mkuu wa Mkoa huo cha kusikiliza kero za wafanyabiashara.
 

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam
 

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari ya Dar es Salaam (TPA)  Mhandisi Juma Javara amewaondoa shaka wafanyabiashara wanaotumia bandari hiyo kwa kuwahakikishia kuwa sasa hakuna ucheleweshaji wa kutoa makontena ya mizigo bandarini hapo.

Kauli hiyo ameitoa jijini Dar es Salaam wakati akijibu maswali kutoka Jumuiya ya Wafanyabiashara wa jijini humo katika Kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam cha kusikiliza kero za Wafanyabiashara kilichokutanisha Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Manispaa, Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini (TPSF), Uhamiaji, Mameneja wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Maafisa wa TPA  na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Amesema kuwa kutokana na maboresho yaliyofanyika bandarini hakuna meli za mizigo zinazokaa muda mrefu zikisubiri kushusha mizigo iliyo kwenye makontena na bidhaa nyingine katika bandari hiyo.

" Niwaondoe shaka wafanyabiashara sasa hivi meli za kontena hazikai zaidi ya siku 7 bandarini mizigo inatolewa kwa haraka sababau ya maboresho yaliyofanyika," amesema Mhandisi Javara.

Amebainisha kuwa Rais Samia Suluhu Hassan alitoa Sh Bilioni 12 kwa ajili ya maboresho na ununuzi wa vifaa ambapo kwa kiasi kikubwa zimepunguza malalamiko ya ucheleweshaji wa kutoa mizigo bandarini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa huo, RC Makalla amesema majibu yote yaliyotolewa na TPA, TRA Uhamiaji  na mamlaka nyingine yatawekwa kwenye maandishi na nakala itapelekwa katika jumuiya hiyo.

Pia RC Makalla amesema Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Hassan Rugwa ataongoza kamati hiyo itakayojumuisha watu wa TPA, TRA, Uhamiaji, Ofisi ya Rais na mamlaka nyingine ambapo itakuwa na jukumu la kukutana na wafanyabiashara kujadili mambo mbalimbali.
   

No comments:

Post a Comment

Pages