May 20, 2022
MOROCCO IACHE KUIKALIA SAHARA MAGHARIBI KIMABAVU
Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali ya Morocco kuacha kuikalia kimabavu Nchi ya Sahara Magharibi kinyume na sheria za kimataifa na haki ya Nchi kujitawala na kujiamulia mambo yake (right of sovereignty).
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ndugu Ado Shaibu kwenye Maadhimisho ya Miaka 100 ya Kuzaliwa kwa Mwalimu Julius Nyerere yaliyoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere (The Mwalimu Nyerere Foundation) katika Hotel ya Four Points, Dar es salaam leo tarehe 17 Mei, 2022.
"Ninafurahi kuyasema haya mbele ya Balozi wa Sahara Magharibi Ndugu Mahyub Sidina na Maafisa Waandamizi wa Ubalozi wa Morocco ambao mmehudhuria maadhimisho haya. Tanzania, kwa mujibu wa Mwalimu Nyerere, haiwezi kusemwa kuwa iko huru kama kuna Nchi yoyote ndani ya Afrika inaendelea kutawaliwa"-alisema Ndugu Ado Shaibu.
"Kitendo cha Morroco kuendelea kuikalia Sahara Magharibi kimabavu tangu Mwaka 1975 hakikubaliki. Tunatoa wito wa kufanyika kura ya maoni ya Wananchi wa Sahara Magharibi kuamua hatma yao kama ilivyoazimiwa na Umoja wa Mataifa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kura ya Maoni ya Sahara Magharibi (MINURSO) ukaundwa Mwaka 1991"
Maadhimisho ya Miaka 100 ya Kuzaliwa kwa Mwalimu Nyerere yalihudhuriwa na Viongozi Mbalimbali wa Serikali, Mabalozi, Wanazuoni, Asasi za Kiraia na Viongozi wa Vyama vya Kisiasa.
No comments:
Post a Comment