May 20, 2022

PROFESA KIKULA AAINISHA MAFANIKIO MAKUBWA USHIRIKISHWAJI WA WATANZANIA SEKTA YA MADINI


Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula ameeleza kuwa tangu kuanza kwa utekelezaji wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 ambayo ilipelekea kutungwa kwa kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini za Mwaka 2018 mafanikio makubwa yamepatikana ikiwa ni pamoja na ongezeko la fursa za uwekezaji katika sekta ya madini, teknolojia, manunuzi na ajira na kupelekea Sekta ya Madini kuendelea kukua kwa kasi.
 
Profesa Kikula ameyasema hayo leo tarehe 20 Mei, 2022 alipokuwa akitoa hotuba kwa niaba ya Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko kwenye ufunguzi wa Jukwaa la Kwanza la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini jijini Mwanza ambalo limekutanisha wadau wa madini kwa ajili ya kupata elimu kuhusu ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya madini pamoja na kujadili changamoto mbalimbali.
 
Akielezea mafanikio hayo, Profesa Kikula ameeleza kuwa tangu kuanza kwa  usimamizi wa ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini ajira kwa kwa watanzania katika migodi mikubwa na ya kati zimeongezeka kutoka 6,668 sawa na asilimia 95 kwa Mwaka 2018 hadi kufikia 14,308 sawa na asilimia 97 kwa Mwaka 2021 ya ajira zote, ongezeko lililochangiwa na watanzania kupewa kipaumbele kwenye ajira zote nchini.
 
Amefafanua mafanikio mengine kuwa ni pamoja na ongezeko la kiwango cha  manunuzi ya bidhaa na huduma zinazotolewa na watanzania na kampuni za kitanzania ambapo kiwango hicho katika mwaka 2018 kilikuwa ni jumla ya Dola za Kimarekani milioni 238.71 sawa na asilimia 46 ya manunuzi yote, na mwaka 2021 kufikia jumla ya Dola za Kimarekani bilioni 2.104 sawa na asilimia 97 ya manunuzi yote.
 
Amesema kuwa, kumekuwa na ongezeko la idadi ya watoa huduma watanzania na kampuni za kitanzania ambapo kwa mwaka 2021 jumla yake ilifikia 961 sawa na asilimia 61 ya watoa huduma wote katika kipindi hicho.
 
Ameendelea kusema kuwa katika kipindi cha kuanzia Mwaka 2018 hadi 2021, uelewa wa masuala ya Ushirikishwaji wa Watanzania umeongezeka kwa kiasi kikubwa na kuchochea wadau wengi katika Sekta ya Madini kutimiza matakwa ya Kisheria.
 
“Uelewa umeongezeka miongoni mwa watanzania kwa kuona fursa mbalimbali ambazo wanaweza kuzichukua na kuwanufaisha, vilevile uelewa katika kampuni za kigeni umeongezeka na baadhi ya kampuni hizo zimekwisha kukamilisha uwasilishaji wa mipango ya Ushirikishwaji wa Watanzania na uundaji wa Kampuni za ubia na Kampuni za Kitanzania”, amesema Profesa Kikula.
 
Aidha, ameeleza mafanikio mengine kuwa ni pamoja na ukuaji wa teknolojia katika Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa matumizi  ya mitambo yenye uwezo mkubwa katika uzalishaji na hivyo kupelekea kuongeza uzalishaji kwa kiasi kikubwa.
 
Ameongeza kuwa katika  eneo la teknolojia mambo kadhaa yamefanyika ikiwa ni pamoja na kuwajengea wazanzania uwezo  wa kufanya kazi mbalimbali kwa kutumia teknolojia ambazo hapo awali hazikuwepo nchini.
 
Katika hatua nyingine amesema kuwa katika kipindi cha kuanzia Mwaka 2018 hadi 2022, shughuli za utafiti na maendeleo katika Sekta ya Madini nchini zimeongezeka na kupelekea uanzishwaji wa miradi mikubwa ya uchimbaji mkubwa wa madini nchini na uwepo wa njia bora za kufanya uzalishaji, uchenjuaji, usafishaji, ukataji na usanifu wa madini.
 
Naye Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga akizungumza kwenye jukwaa hilo sambamba na kupongeza kazi kubwa inayofanywa na Tume ya Madini kwenye usimamizi wa ushirikishwaji wa watanzania kwenye Sekta ya Madini ameitaka Tume ya Madini kuendelea kutoa elimu kwa wadau wote wa madini nchini ili washiriki kikamilifu na kupata faida huku wakilipa kodi mbalimbali serikalini.
 
Amesisitiza kuwa serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika Sekta ya Madini kwa wananchi, na kuwataka kuchangamkia fursa mbalimbali ikiwemo utoaji huduma kwenye migodi ya madini kama vile vyakula, ulinzi, ajira, uuzaji wa bidhaa mbalimbali n.k.
 
Naye Kamishna wa Tume ya Madini, Janet Reuben Lekashingo amewataka wananchi kuchangamkia fursa za uwekezaji katika sekta ya madini hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zenye madini  mengi hususan ya dhahabu.
 
Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba ameongeza kuwa lengo la kuwa na jukwaa la kwanza la utekelezaji wa ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya madini ni kuwajengea uwezo wadau wa madini na kushiriki kikamilifu kwenye shughuli zote za madini nchini.
 
Amesisitiza kuwa, Tume ya Madini itaendelea kutoa elimu katika maeneo mengine katika Sekta ya Madini lengo likiwa ni kuhakikisha shughuli za madini zinafanyika kwa ufanisi huku mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa ukiendelea kukua.
 
Wakati huohuo, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Kanali Denis Mwila akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel ameipongeza Wizara ya Madini kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini mkoani Mwanza na kuongeza kuwa kumekuwepo na ongezeko kubwa la ushiriki wa watanzania kweye shughuli za madini na kusisitiza kuwa uchumi wa madini unakwenda kuongezeka kutoka asilimia 7 hadi 10 ifikapo mwaka 2025.


Kabla ya ufunguzi wa jukwaa hilo, Profesa Kikula ametembelea mabanda ya Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Madini na ya wadau wa madini kwenye maonesho yanayoendelea ikiwa ni sehemu ya mkutano huo.

No comments:

Post a Comment

Pages