June 10, 2022

KAMPUNI ZA T-PESA NA NGASMAKE CO. LTD KUWALINDA WANUNUZI NA WAUZAJI BIDHAA MTANDAONI

Mkurugenzi Mtendaji wa Ngasmake Co. Ltd, Bw. Emmanuel Ngalya (kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa T-PESA, Bi. Lulu Mkudde wakizinduwa rasmi ushirikiano wao wa huduma ya 'Lipa kwa Uhakika' inayomwezesha mteja wa T-Pesa kufanya malipo salama ya bidhaa mtandaoni bila kutapeliwa. Mfumo huo wa malipo ya fedha unamlinda mnunuzi na muuzaji kwa pamoja pia. Hafla hiyo imefanyika leo Makao Makuu ya TTCL, jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa T-PESA, Bi. Lulu Mkudde akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa ushirikiano wao wa huduma ya 'Lipa kwa Uhakika' inayomwezesha mteja wa T-Pesa kufanya malipo salama ya bidhaa mtandaoni bila kutapeliwa. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Ngasmake Co. Ltd, Bw. Emmanuel Ngalya (wa kwanza kushoto) akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa ushirikiano wao wa huduma ya 'Lipa kwa Uhakika' inayomwezesha mteja wa T-Pesa kufanya malipo salama ya bidhaa mtandaoni bila kutapeliwa. Katikati ni Mkurugenzi wa T-PESA, Bi. Lulu Mkudde pamoja na Meneja Mahusiano wa TTCL, Bw. Edwin Mashasi.

Na Joachim Mushi, Dar 

KAMPUNI ya T-PESA kwa kushirikiana na Kampuni ya Ngasmake Co. Ltd wameingia makubaliano ya kibiashara ambapo sasa wateja wa T-PESA kufanya malipo ya bidhaa mtandaoni kwa usalama kwa kutumia mfumo wa malipo ya fedha 'Lipa kwa Uhakika' unaomlinda mnunuzi na muuzaji kwa pamoja.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa ushirikiano huo,  Mkurugenzi Mtendaji wa Ngasmake Co. Ltd, Bw. Emmanuel Ngalya alisema kutokana na maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano kumerahisisha mambo hasa ufanyaji biashara kupitia mitandao ambapo pia umekuwa na changamoto ama za kutapeliana fedha kwa mnunuzi au bidhaa kwa muuzaji.

Alisema Kampuni ya Ngasmake Co. Ltd kwa kushirikiana na T-PESA imekuja na suluhisho la changamoto hiyo kwa kutambulisha 'Lipa kwa Uhakika' ambapo sasa itapatikana kupitia menyu ya T-PESA, na mteja atakaponunua bidhaa mtandaoni na kulipa kupitia mfumo huu hela itahifadhiwa kwa muda kabla ya kumfikia muuzaji ili kuleta usalama wa pande mbili.

"Mfumo wa Lipa kwa Uhakika unavyofanya kazi, mnunuzi baada ya kununua bidhaa na kulipia kupitia T-PESA, fedha hizo hazitaenda moja kwa moja kwa muuzaji zitaifadhiwa kwenye mfumo mpaka mnunuzi atakapopata bidhaa yake na kudhibitisha ni bidhaa yenyewe aliyoagiza ndio mfumo utaruhusu fedha hizo kwenda kwa muuzaji," alisema Bw. Ngalya.

"...Kutokana na changamoto hiyo ndio maana kampuni ya Ngasmake imekuja na suluhisho ya kuja na mfumo rafiki na salama wa Lipa kwa Uhakika utakaomsaidia mnunuzi na muuzaji kuwa salama katika biashara za mtandao (online business) na kuondoa changamoto ya udanganyifu, utapeli na kupata bidhaa zisizo na kiwango. Huduma hii inatoa fursa kwa mnunuzi na muuzaji kupata huduma ya uhakika na kuweka mazingira salama ya kifedha kwa mnunuzi na muuzaji." alisema Mkurugenzi huyo Mtendaji wa Ngasmake Co. Ltd.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa T-PESA, Bi. Lulu Mkudde alisema nchi ya Tanzania inajivunia uwepo wa miundombinu rafiki ya mawasiliano yenye uwezo mkubwa wa kutosheleza mahitaji ya watumiaji nchini, na ndiyo maana T-PESA imewezesha huduma ya Lipa kwa Uhakika ambayo ni ya kipekee kabisa inayowahakikishia usalama wa bidhaa zao. 

Alisema T-PESA imeupokea kwa furaha mfumo wa Lipa kwa Uhakika kwani unakwenda kumaliza kilio cha muda mrefu cha wanunuzi wa bidhaa kutopata bidhaa zao ilihali wanakua wameshafanya malipo, lakini kupitia mfumo huo utazuia udanganyi na utapeli huo.

"Kampuni ya T-PESA inapenda kutoa rai kwa wanunuzi wa huduma au bidhaa kupitia mitandao ya kibiashara inayopatikana nchini kutumia mfumo wa Lipa kwa Uhakika ambapo unatoa usalama wa fedha zao. Napenda kutumia fursa hii kuwaambia makampuni au watu binafsi wenye mawazo ya kibunifu hasa kwenye sekta ya mawasiliano kuja T-Pesa kwani mifumo yetu ni salama na ni ya uhakika." alisisitiza Bi. Mkudde akizungumza na wanahabari.

No comments:

Post a Comment

Pages