Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dkt. Wilson Mahera Charles.
********
WATANZANIA
wametakiwa kuwa tayari kushiriki kikamilifu zoezi la kuhesabiwa wakati wa sensa
ya watu na makazi itakayofanyika tarehe 23 agosti, 2022, nchini kote. Wito huo
umetolewa jana na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dkt.
Wilson Mahera Charles ofisini kwake jijini Dodoma. Amesema zoezi la Sensa ya watu na makazi ni
muhimu kwa maendeleo ya nchi kwani hata Tume ya Taifa ya Uchaguzi hutegemea
takwimu za sensa kukadiria idadi ya wapiga kura wapya watakaoandikishwa pamoja na
waliopoteza sifa za kuandikishwa kama vile waliofariki. “Kimsingi wapiga kura au shughuli za uchaguzi kwa
ujumla zina uhusiano mkubwa na takwimu zitokanazo na sensa, kwani katika sensa
ndipo Tume inaweza kubainisha idadi ya watu itakayowaandikisha katika daftari
la kudumu la mpiga kura,”amesema Dkt. Mahera na kuongeza: “Nawahimiza
watanzania kujitokeza kuhesabiwa kwenye sensa ya watu na makazi mwaka huu na
kila mmoja kumhamasisha mwenzake kuhesabiwa.” Dkt Mahera
amesisitiza kuwa ili
Tume iweze kufanya shughuli zake vizuri ni lazima ipate takwimu sahihi za watu,
makazi na kutambua makundi maalum ambayo ni ya wanawake, wazee, vijana na watu
wenye ulemavu. Mkurugenzi wa
Uchaguzi ameongeza kuwa kutokana na sensa ya mwaka huu kufanyika kwa kutumia
teknolojia ya kisasa ambayo itawezesha kutambua idadi ya majengo ya umma na
makazi ya watu, Tume inatarajia kutumia takwimu hizo, kuweka vituo vya
uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga kura. “Sensa ya mwaka
huu itafanyika kidijiti na itaweza kubainisha idadi ya majengo ya umma ambayo
sisi huyatumia kuweka vituo vya kujiandikisha, lakini pia itatusaidia pia kuweka
vituo hivyo kwa mujibu wa anuani za makazi ambazo pia sensa inakwenda
kuzitambua rasmi,” amesema Dkt Mahera. Pia Dkt Mahera
amesema Tume imekua ikipanga mipango yake kwa takwimu kuanzia ngazi ya kata
lakini sasa kwa kuwa sensa inakwenda kuweka kumbukumbu hadi ngazi ya kitongoji,
Tume itaweza kupanga mipango yake kwa urahisi zaidi na matumizi ya teknolojia
katika uchaguzi yataongezeka. Sensa ya watu
na makazi hufanyika kila baada ya miaka 10 na mara ya mwisho Sensa hiyo ilifanyika
mwaka 2012 ambapo watanzania milioni 44,929 walihesabiwa.
No comments:
Post a Comment