June 19, 2022

Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar akutana na Balozi wa Uingereza

MAKAMU wa Kwanza wa Rais  wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, amesema kuna umuhimu mkubwa Zanzibar kufikiria kuunda chombo rasmi kitakachopewa jukumu la kisheria, kusimamia, kuangalia na kupima utekelezaji wa masuala yote yanayohusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.



Mhe. Othman, ameyasema hayo ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar, alipokutana na Balozi mdogo wa Uingereza nchini Tanzanbia Rick Shearn, aliyetaka kufahamu maendeleo utekelezaji wa  masuala mbalimbali ya uimarishaji wa demokrasia pamoja na serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.  


Mhe. Makamu amefahamisha kwamba kuwepo kwa chombo hicho kutasaidia sana kuziona changamoto na kupanga kwa pamoja namna bora ya kuzipatia ufumbuzi ili serikali hiyo iweze kuendelea na kuwa na manufaa zaidi kwa Zanzibar.

Amefahamisha kwamba suala hilo ni miongoni mwa mapendekezo kadhaa yaliyowasilishwa serikalini kwa ajili ya kujadiliwa ili yatakapokubalika hatua rasmi za kuundwa kwa chombo cha aina hiyo ziweze kuchukuliwa.


Aidha amesema kwamba katika kuendeleza suala hilo la serikali ya Umoja wa Kitaifa kunahitajika pia kuitishwa makongamano ya kitaifa ili kupata maoni na fikra mbali mbali za wananchi katika kuweka mkakati bora wa serikali hiyo.


Amesema kwamba yapo masuala mengi yanayoainishwa  kwa nia ya kuyafanyia mageuzi makubwa ikiwemo tume ya Uchaguzi kwa kuwa matumaini ya wananchi ni kuwepo mabadiliko ya kweli katika masuala mbali mbali hasa mambo yanayohusu uchaguzi.


Amefahamisha kwamba kutokana na kukosekana utulivu wa kisiasa Zanzibar imepoteza mambo mengi ikiwemo misaada ya maendeleo na kusisitiza kwamba wananchi hawana budi kuwa wavumilivu wakati viongozi wakiendelea na juhudi kubwa za kujenga mustakabali  mwema wanchi yao.

Naye Balozi mdogo  wa Uingereza nchini Tanzania  Bwana Rick Shearn, alisema shughuli za maendeleo ya kiuchumi na uwekezaji zinahitaji sana hali bora, utulivu  na mazingira mazuri ya kisiasa na kwamba kuwepo serikali ya Umoja wa kitaifa kunasaidia sana kuleta utulivu  Zanzibar na Tanzania kwa jumla.


Akizungumzia tatizo la dawa za kulevya, Balozi huyo alieleza kwamba nchi yake  itaendelea kusaidia Zanzibar kwa kuijengea uwezo Mamlaka pamoja na watendaj katika Mamlaka hiyo  ya Kupambana na kudhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar ili suala hilo liweze kufanikiwa.


No comments:

Post a Comment

Pages