June 16, 2022

MASHIRIKA YA UMMA YANAYOTEGEMEA RUZUKU YAAGIZWA KUANDAA MIKAKATI


Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) wakiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ta Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.

 

 Na Peter Haule, WFM, Dodoma

 

Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, amemuagiza Waziri wa Fedha na Mipango na Msajili wa Hazina kuhakikisha mashirika ambayo yanategemea ruzuku kutoka mfuko Mkuu wa Serikali kuja na mikakati madhubuti na inayotekelezeka ya kupunguza utegemezi kwa Serikali.

Mhe. Makamu wa Rais, ametoa agizo hilo jijini Dodoma baada ya kupokea gawio la kiasi cha shilingi bilioni 30.7 zilizotolewa na Benki ya NMB ikiwa ni mapato ya Serikali yanayotokana na uwekezaji wa hisa asilimia 31.8 kwenye benki hiyo.  

Makamu wa Rais amemuagiza Waziri wa Fedha na Mipango na Msajili wa Hazina kuwabana wakuu wa taasisi husika watekeleze agizo hilo au kupitia Waziri wa Fedha na mipango awasilishe kwa Mamlaka mapendekezo ya kuwawajibisha watendaji.

“Taasisi zinazotakiwa kutoa asilimia 15 ya mapato ghafi kwa mujibu ya Sheria zinatakiwa kufanya hivyo kikamilifu na kwa wakati na Bodi na Menejimenti za Mashirika ambayo yamekuwa yanasuasua katika uendeshaji, hayachangii katika mfuko Mkuu wa Serikali na hayana mchango katika maendeleo ya nchi Waziri wa Fedha uwatathimini kama kweli wanatosha kwenye nafasi zao na ulete mapendekezo kwa mamlaka”, alisema Mhe. Mpango.

Alisema kuwa fedha ambazo Serikali imewekeza kwenye taasisi ni fedha za wananchi na Serikali inayowajibu kuhakikisha fedha zinazalisha na gawio linatolewa kwa manufaa ya wananchi wenyewe.

Alisisitiza kuwa mashirika yote, taasisi na Wakala wa Serikali zihakikishe zinakidhi matakwa ya Sheria ya Msajili wa Hazina ya kuhakikisha gharama za uendeshaji hazivuki viwango vilivyowekwa kisheria kwa kuwa bado kuna taasisi na mashirika ya umma ambayo ushiriki wake katika uchangiaji umekuwa wa kusuasua huku wakitoa visingizio lukuki.

Alisema Serikali ya Awamu ya sita itaendelea kuimarisha na kuweka mazingira rafiki na endelevu ya kufanya biashara katika sekta ya fedha na sekta nyingine zote.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, awali alisema kuwa Wizara yake itaendelea kushirikiana na taasisi zote za sekta binafsi na taasisi ambazo Serikali ina hisa ili kuhakikisha zinafanya kazi vizuri zaidi

Alisema kuwa, Mhe. Rais amefungua uchumi kwa kiwango kikubwa na matokeo yake ni kila sekta inapata matunda.

Naye Msajili wa Hazina Bw. Mgonya Benedict, alisema kuwa hadi sasa Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia mashirika, Wakala za Serikali, taasisi za Umma na Kampuni ambazo Serikali inahisa 287, ambapo mwaka 2020/21 Ofisi ya Msajili wa Hazina ilikusanya mapato yasiyo ya kodi jumla ya shilingi bilioni 637 na katika mwaka unaoendelea 2021/22 imekusanya takribani shilingi bilioni 734 sawa na ongezeko la asilimia 15.2 ukilinganisha na mwaka wa fedha uliotangulia.

Alisema ongezeko hilo linachangiwa na usimamizi Madhubuti, ufuatiliaji na tathimini ya uwekezaji wa mitaji ya umma ambapo majukumu ya Msajili wa Hazina kama yalivyoainishwa kwenye Sheria yake SURA 370 ni pamoja na kushauri na kusimamia uwekezaji katika mashirika, wakala za Serikali na taasisi za umma, kampuni ambazo Serikali ina hisa chache na kuhakikisha uwekezaji unaleta tija kwa kutoa gawio na michango mingine Serikalini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NMB, Dkt. Edwin Mhede, alisema Benki ya NMB ipo mstari wa mbele kuhakikisha inatafsriri Sera vizuri kwa kutoa mikopo kwa sekta binafsi na huduma bora hivyo gawio lililotolewa kwa Serikali ni uthibitisho wa utekelezaji huo.

Aliipongeza Serikali kwa namna inavyosimamia sekta ya fedha kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kuifanya iwetulivu na kutofanya mambo kiholela.

Alisema kuwa sekta ya fedha isiyosimamiwa ipasavyo inaweza kusababisha kutopata matokeo yanayotarajiwa hivyo inahitaji kudhibitiwa ili kuweza kutekeleza mambo kwa ufanisi.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna, alisema kuwa gawio la Serikali kutoka Benki ya NMB limeendelea kukua kila mwaka kutoka bilioni 10.48 mwaka 2018 mpaka bilioni 30.7 kwa sasa ambapo ni mafanikiao makubwa yanayotokana na maendeleo chanya ya kiutendaji ya benki hiyo.

Alisema kuwa Benki hiyo imeweza kuongeza mtaji wa hadi kufikia shilingi trilioni 1.3 na uwiano kati ya gharama za uendeshaji na mapato ulikuwa asilimia 60 miaka mitatu iliyopita, kwa mwaka 2021 uwiano ulikuwa asilimia 46 na sasa ni asilimia 42 wakati kiwango cha BOT ni angalau chini ya asilimia 55.

Mkutano wa mwaka wa 22 uliofanyika Juni 3, 2022 wanahisa wa Benki ya NMB waliidhinisha gawio la shilingi 193 kwa kila hisa ambayo ni sawa na jumla ya shilingi bilioni 96.7 ili ziweze kulipwa kwa mwaka 2021 kwa wanahisa wa benki hiyo ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 41 kutoka shilingi bilioni 68.5 ambazo zililipwa kama gawio mwaka 2020.

No comments:

Post a Comment

Pages