Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) inamshikilia muuguzi msaidizi katika zahanati iliyopo Kariakoo jijini Dar es Salaam, Salum Mpangula kwa tuhuma za kukutwa na kilo 174.77 ya dawa za kulevya.
Mpangula alikamatwa na dawa hizo Mei 12 nyumbani kwake Tabata relini jijini Dar es Salaam zikiwa zimefungwa kwenye paketi 162.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 3, 2022 jijini hapa Kamishna Jenerali wa DCEA, Gerald Kusaya amesema kufuatia upekuzi uliofanyika nyumbani kwa mtuhumiwa huyo, paketi 162 zenye unga uliodhaniwa kuwa dawa za kulevya zilikutwa ndani ya viroba sita vilivyokuwa vimehifadhiwa chumbani kwa mtuhumiwa huyo.
Amesema paketi moja ya unga huo ilikuwa imewekwa kwenye mfuko mweusi wa nailoni na kufichwa chini ya kitanda.
"Taarifa ya uchunguzi wa kitaalam kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali imethibitisha kuwa paketi zote 163 zilikuwa na dawa za kulevya aina ya heroin ambazo jumla yake ni Kilogramu 174.77.
"Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya taratibu za kisheria kukamilika. Kwa upande wa kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya," alisema
Aidha Kamishna Jenerali Kusaya amesema mamlaka hiyo imekamata jumla ya kilogramu 877.217 za dawa za kulevya na kuzuia uingizaji wa kilogramu 122,047.085 na Lita 85 za kemikali bashirifu nchini.
Amesema kati ya dawa hizo ni heroin kilogramu 174.112 zilizowahusisha watuhumiwa wawili na bangi kilogramu 703.105 zilizowahusisha watuhumiwa sita ambao wote wamefikishwa mahakamani.
"Mamlaka inaendelea kufanya kaguzi za kufuatilia watu wanaokiuka taratibu za uingizaji na
usambazaji wa kemikali bashirifu na dawa hizo ili kuzuia uchepushwaji. ambapo katika
kipindi hicho kupitia mfumo wa kielektroniki (PEN-ONLINE SYSTEM) mamlaka ilifanikiwa kuzuia uingizaji wa kilogramu 122,047.085 na Lita 85 za kemikali bashirifu," amesema
Aidha, amesema mamlaka imeteketeza jumla ya hekari 21 za mashamba ya bangi mkoani Arusha
na jumla ya kilogramu 250.7 za dawa za kulevya aina ya heroin na cocaine ambazo mashauri yake yalimalizika mahakamani, katika kiwanda cha saruji cha Dangote mkoani Mtwara.
Amesema katika kuhakikisha jamii inapata elimu sahihi juu ya tatizo la dawa za kulevya, Mamlaka
imeandaa muongozo utakaotumika kutoa elimu, imeshiriki kuandaa ujumbe juu ya tatizo la dawa za kulevya katika Mbio za Mwenge wa Uhuru zinazoendelea na kutoa elimu.
Aidha amesema Juni 26 ya kila mwaka, Tanzania huungana na Mataifa mengine kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya Duniani.
Amesema lengo likiwa ni kuongeza uelewa wa jamii na kuhamasisha Umma kushiriki katika mapambano dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya.
"Mwaka huu Kitaifa maadhimisho haya yatafanyika jijini Dar es Salaam, katika viwanja
vya Mnazi Mmoja na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa.
Kauli mbiu ya maadhimisho haya ni “Tukabiliane na changamoto za dawa za kulevya kwa ustawi wa jamii”.
"Maadhimisho haya kwa mwaka huu yatafanyika kuanzia Juni 30, mwaka huu kwa utoaji elimu na maonesho ya shughuli mbalimbali za udhibiti zinazofanywa na wadau mbalimbali katika udhibiti wa dawa za kulevya ambapo kilele chake kitakuwa siku ya Jumamosi Julai 02 mwaka huu," amesema
No comments:
Post a Comment