Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, akipokea tuzo maalum kutoka kwa Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Mahakama ya Tanzania, Beatrice Patrick, iliyotolewa na Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (UTUMISHI) kwa
kushinda nafasi ya pili (2) kati ya Idara zinazojitegemea 26 kwa
utendaji mzuri katika usimamizi wa rasilimaliwatu kwa kufuata Sheria,
Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2021/2022.
Na Mwandishi Wetu
Mahakama ya Tanzania imepewa tuzo maalum na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (UTUMISHI) kwa kushinda nafasi ya pili (2) kati ya Idara zinazojitegemea 26 kwa utendaji mzuri katika usimamizi wa rasilimaliwatu kwa kufuata Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2021/2022.
Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi tuzo hiyo kwa Mtendaji Mkuu wa MahakamacMkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu- Mahakama ya Tanzania, Beatrice Patrick amesema kuwa tuzo hiyo ilitolewa katika kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo vya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wote kutoka Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Mikoa; Majiji, Miji na Halmashauri, Taasisi za Serikali kama Vyuo, Vyuo Vikuu na Mashirika ya Umma kilichofanyika jijini Dodoma hivi karibuni.
“Nipo hapa kwa lengo la kukabidhi tuzo maalum iliyotolewa kwa Mahakama katika kikao ambacho uliniagiza na kunipa ruhusa ya kuhudhuria, katika kikao hiki Mgeni Rasmi Mhe. Jenista Mhagama, Waziri-UTUMISHI alitoa tuzo kwa Taasisi za umma ambazo zimekuwa na utendaji mzuri, hivyo Mahakama ilifanikiwa kushika nafasi ya pili kwenye kundi la Idara Zinazojitegemea baada ya Tume ya Uchaguzi kushika nafasi ya kwanza na Ofisi ya Bunge kuwa wa tatu,” amesema Beatrice.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa, utoaji wa Tuzo hizo umezingatia vigezo kadhaa ikiwemo; kutumia vema Mfumo wa Taarifa za Kumbukumbu na Mishahara ya Watumishi (HCMIS) na kuhamisha kwa mafanikio na kwa wakati taarifa za watumishi kutoka mfumo wa ‘Lawson’ kwenda Mfumo wa ‘HCMIS’ usahihi wa taarifa za watumishi katika Mfumo huo.
Ametaja vigezo vingine ni pamoja na; kupungua kwa idadi ya malalamiko ya watumishi yanayopelekwa UTUMISHI kupitia mfumo/utaratibu wa ‘e-mrejesho’ na uwepo wa malalamiko yaliyosajiliwa; kushughulikia ipasavyo na kutekeleza kwa wakati maelekezo na masuala mbalimbali ya kiutumishi yanayotolewa na UTUMISHI na haiba na utendaji kazi mzuri.
Kigezo kingine ni Uzingatiaji wa maadili na kushughulikia mashauri ya nidhamu kwa wakati na kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amekiri kufurahishwa na tuzo hiyo na kuahidi kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Kwetu sisi Mahakama, hii tuzo ni kitu kikubwa sana na tunathamini na hii itatupa nguvu ya kuendelea kufanya vizuri zaidi ili wananchi waendelee kunufaika na huduma tunazozitoa,” amesema Prof. Ole Gabriel.
No comments:
Post a Comment