June 10, 2022

Mwalimu Benki yaanzisha ‘Jenga na Mwalimu’

Meneja Biashara wa Benki ya Mwalimu, Sabina Mwakasungura akizungumza na waandishi wa habari.

Kaimu Mkurugenzi wa Benki ya Mwalimu, Abdallah Kirungi (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa vifaa vya ujenzi FMJ ‘wahenga’, Fatina Senzota wakisalimiana.


 Kutoka kushoto ni Mshauri wa ufundi wa bidhaa ya Jenga na Mwalimu Benki, Wema Muhama, Mkurugenzi Mkuu wa wauzaji wa vifaa vya ujenzi FMJ ‘Wahenga’, Fatina Senzota, Kaimu Mkurugenzi wa Mwalimu Benki, Abdallah Kirungi na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Biashara na Masoko wa Mwalimu Benki, Sabina Mwakasungura wakizungumza na waandishi wa habari kuhusu bidhaa ya Jenga na Mwalimu Benki.

Na Irene Mark

BENKI ya Biashara ya Mwalimu imezindua bidhaa ya Jenga na Mwalimu Bank itakayomsaidia mwalimu kupata mkopo wa vifaa vya ujenzi ili aweze kumiliki nyumba ya ndoto yake.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo, Juni 9,2022 Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Biashara na Masoko wa Benki ya Mwalimu, Sabina Mwakasungura alisema bidhaa hiyo ni maalum kwa walimu na wajasiriamali kukopeshwa vifaa vya ujenzi ili kufikia lengo la kumiliki nyumba na kuboresha makazi yao kwa bei nafuu.

Mwakasungura alisema benki hiyo inatolewa kwa ushirikiano na Kampuni kongwe ya vifaa vya ujenzi, FMJ Hardware Ltd ‘Wahenga’ ambao ni wauzaji wa vifaa vya ujenzi ndani na nje ya nchi kwa bei ya jumla.

Kwa mujibu wa Mwakasungura, bidhaa hiyo itawasaidia wateja wake kuunganishwa na huduma za maji na umeme.

“...Katika kuhakikisha usalama wa vifaa hivyo, Mwalimu Benki itaviwekea bima ya uharibifu kipindi cha usafirishaji wake kutoka FMJ Hardware hadi kumfikia mteja wetu mahali popote alipo," anasema Mwakasungura.

Alisema benki hiyo inatambua fika kasi ya Serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha Maisha ya watumishi wa umma hususani walimu.

"Benki yetu haiko mbali katika kuunga juhudi hizi kwa kutoa huduma za kifedha kwa gharama nafuu ili kuhakikisha wafanyakazi wanaishi katika mazingira bora na hatimaye kufanya kazi kwa ufanisi," alisisitiza Mwakasungura.

No comments:

Post a Comment

Pages