June 21, 2022

TRA YABORESHA MFUMO WA MASHINE ZA EFD

Na Farida Ramadhani na Peter Haule, WFM, Dodoma

 

Serikali imeeleza kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeboresha mfumo wa usimamizi wa mashine za kutolea risiti za kielektroniki (EFD) kwa kuuwezesha kupokea taarifa zote za kila risiti inayotolewa na kuitunza katika seva zake ili kuwezesha nakala ya risiti hizo kuweza kupatikana wakati wowote inapohitajika.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande, alipojibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Angelina Adam Malembeka, alietakakujua mpango wa Serikali kuboresha stakabadhi za mashine za EFD ili zisifutike baada ya muda mfupi.

Mhe. Chande alisema kufutika kwa stakabadhi hizo baada ya muda mfupi kunasababishwa na matumizi ya karatasi zenye ubora hafifu na kubainisha kuwa karatasi zinazopaswa kutumika ni zile zenye ubora wa "thermal paper".

“Shirika la Viwango Nchini (TBS) kwa kushirikiana TRA imeshatengeneza viwango vya ubora wa karatasi hizo vinavyotakiwa na kwa sasa wanaendelea na usimamizi kuhakikisha karatasi zote zinakidhi ubora unaotakiwa”, alifafanua Mhe. Chande.

Kwa upande mwingine akijibu swali la Mbunge wa Mtoni, Mhe. Abdul-Hafar Idrissa Juma, alietaka kujua wakati ambao Serikali itapeleka fedha za mfuko wa Jimbo katika majimbo ya Zanzibar kwa wakati alisema fedha za mfuko wa Jimbo kwenda Majimbo ya Zanzibar hupelekwa kwa wakati na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za fedha.

“Katika mwaka 2021/22 fedha za mfuko kiasi cha shilingi bilioni 1.4 zimeshatolewa kwa ajili ya majimbo ya Zanzibar”, alibainisha.

Mhe. Chande alisema fedha za mfuko wa Jimbo huhamishwa moja kwa moja kutoka Wizara ya Fedha na Mipango ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenda Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. 

No comments:

Post a Comment

Pages