June 22, 2022

Ushirikiano wa Serikali, MST waokoa vifo 2,800 vya uzazi


Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’ilabuzu Ludigija, akizungumza wakati wa uzinduzi wa kondom za Lifeguard.

 Mkurugenzi wa Marie Stopes Tanzania (MST), Vadacanthara Chandrashekar akizungumza wakati wa uzinduzi wa kondom za Lifeguard.

 

Na Irene Mark

ELIMU na huduma bora za afya ya uzazi zinazotolewa na Shirika la Marie Stopes Tanzania (MST), zimeepusha vifo 2,800 vitokanavyo na uzazi kwa mwaka 2021.

Huduma hizo zimetolewa na MST kwa kushirikiana na Serikali chini ya Wizara ya Afya na kuwafikia wanawake wasiopungua milioni 1.4 kwa mwaka jana wa 2021.

Mkurugenzi wa MST, Vadacanthara Chandrashekar, amesema hayo mwishoni mwa wiki wakati w uzinduzi wa Kondomu za Lifeguard uliohudhuriwa na watu mashuhuri jijini Dar es Salaam akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’ilabuzu Ludigija.

Amesema ushirikiano kati ya
MST na Serikali kumeongeza ufanisi na kuboresha mifumo ya afya nchini kwa kuhakikisha wanawake wengi wanapata huduma bora za afya hususan afya ya uzazi salama.

“Huduma nyingi tunazotoa zipo katika vituo vya afya vya umma kwenye mikoa yote hapa nchini ukiacha ile huduma mkoba ambapo watumishi wetu wa afya wanawafuata wananchi kwenye maeneo yao.

“Mwaka jana 2021 timu yetu ilienda katika vituo vya afya vya umma zaidi ya 5,000 kutoa sindano, vipandikizi na huduma nyinginezo za afya ya uzazi kwa wanawake na wanaume,” alisema Chandrashekar.

Amebainisha kwamba MST inafika kwenye vituo vya afya vya umma kuanzia ngazi ya kijiji hadi wilaya ili kutoa huduma kwa kushirikiana na serikali kuu na serikali za vitongoji.

Chandrashekar anasema uzinduzi wa bidhaa mpya ya Lifeguard ni ishara kwamba wateja bidhaa hiyo wanapata wigo mpana wa kuchagua wapendacho na kufurahia maisha bila maradhi yanayosababishwa na ngono zembe.

“Sio serikali tu, sisi MST tunafanyakazi na washirika wengine wa maendeleo katika kuhimiza matumizi ya vidhibiti mimba nchini…tutaleta bidhaa za kusisimua zaidi ili wanawake na wasichana waweze kutimiza mahitaji yao ya afya ya uzazi,"  anasisitiza Mkurugenzi huyo wa MST.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’ilabuzu Ludigija amesema familia zinatakiwa kujenga utamaduni wa kutumia kondomu ili kujikinga na maradhi yatokanayo na ngono zembe ambayo husababisha kifo na kuacha watoto yatima.

“Mimba zisizotarajiwa na maambukizi ya Ukimwi bado ni makubwa hivyo ni muhimu kutumia kondom hizi za Lifeguard na njia nyingine za uzazi.

“...Ifahamike kwamba hizi bidhaa hasa Lifeguard zinatumiwa na watu wote hadi waliopo kwenye ndoa,” anasisitiza mkuu huyo wa wilaya.

Kwa mujibu wa Ludigija,
maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa vijana katika mikoa mbalimbali ukiwemo wa Dar es Salaam yanaendelea kuongezeka badala ya kupungua.

"Ripoti mbalimbali kutoka kwa wizara ya afya zimeonyesha ongezeko la maambukizi mapya ya VVU kwa asilimia nne," anasema.

Aliwatahadharisha wananchi kuitumia kikamilifu bidhaa hiyo kwani inasaidia kwa njia nyingi ikiwemo kuepusha mimba zisizotarajiwa, mpango salama wa uzazi na kujikinga na magonjwa ya zinaa hasa VVU.

Ludigija anawaonya zaidi vijana aliosema wapo kwenye kundi hatarishi zaidi la kupata VVU kwa kuwa wengi wao wanaongozwa na mihemko pindi wanapokutana na makundi maovu hivyo kujiweka kwenye hatari ya kupata VVU.

“Takwimu mbalimbali za Wizara ya Afya zinaonesha vijana wengi chini ya miaka 40 wapo kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi mapya ya VVU na magonjwa mengine ya ngono, hivyo suala la wao kujilinda na kutambua afya zao ni muhimu kwa kuwa wao ndio wajenzi wa taifa hili.

“Umefika wakati sasa wazazi na walezi washirikiane kutoa elimu kwa vijana wao kuhusu mazingira ya ujana na mihemko yao lakini isitafsiriwe kama ni kuhalalisha uasherati, hapana lengo ni kulinda kizazi cha taifa hili.

“Mbali na vichocheo vya miili yao, pia wanahamasishwa na makundi yenye ushawishi kwao. Kuharibika kizazi cha vijana wa leo maana yake ni kuiharibu Tanzania ya kesho.

“Ningetamani kuona bidhaa hii ya LifeGuard inafika kila kona nchini yetu. Nanyi MST hebu wasikilizeni wanaosema bei za kondom zipo juu, hivyo kama kuna mazingira rafiki ya bei fanyeni maboresho litakuwa jambo zuri, huu ni ushauri wangu kwa wahusika wanasambaza bidhaa hizo,” anasisitiza Ludigija.

Amesma kuwa matumizi ya mipira siyo tu kujikinga na magonjwa ya ngono bali kuna mimba zisizotarajiwa, kupanga familia huku akibainisha kwamba kama familia haina mipango hasa kwenye uzazi mara nyingi husababisha hata uchumi wa kaya husika kuyumba.

“Serikali tunatengeza mazingira ya kufanya matukio kama haya yanayokutanisha vijana wengi, yawe na faida kubwa, kilichobaki ni utekelezaji tu na elimu jinsi ya kutumia hii biadhaa na umuhimu wake,” anasema Ludigija.

Baadhi ya vijana waliohudhuria uzinduzi huo wanasema ujio wa kondom hizo utasaidia hasa kwa vijana wanaosoma vyuo.

“Tunakumbana na vishawishi vingi hasa sisi wasichana kwa hiyo tukiwa na Lifeguard kwenye mkoba ni rahisi kumshawishi utakayekutana nae kuitumia kuliko ukiwa huna kabisa.

“Kuna wakati kondom ziliadimika kabisa naamini ukifanyika utafiti itabainika wasichana wengi wa vyuo walipata maradhi na mimba zisizotarajiwa,” anasema Vanessa Edward mwanachuo kutoka mkoani Morogoro.

Hata hivyo wameishauri serikali kuhakikisha kondom za Lifeguard zinafika vyuoni na kusambazwa kwa wanavyuo bila gharama au kwa kiasi kidogo cha fedha ili kuchangia.

No comments:

Post a Comment

Pages