June 15, 2022

WAZIRI MULAMULA ASISITIZA UMOJA NA MSHIKAMANO KWA NCHI ZA AFRIKA NA NORDIC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amesisitiza umoja na mshikamano kwa nchi za Afrika na Nordic aliposhiriki Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nchi za Nordic uliofanyika tarehe 14 Juni 2022 jijini Helsinki, Finland.


Mkutano huo ulifunguliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Mhe. Pekka Haavisto ambapo aliwakaribisha wajumbe wa mkutano huo kushiriki mjadala wa vijana wa Nordic – Afrika pamoja na ajenda nyingine za majadilianao baina ya mawaziri hao.

 

Akichangia mjadala wa vijana Mhe. Waziri Mulamula amewasihi vijana waliopata nafasi ya kushiriki katika masuala mbalimbali ya kimataifa kujitoa kwa dhati ili kuleta tija katika nchi zao pamoja na kusaidia vijana wengine kupata nafasi hizo.

 

Sambamba na hilo katika nafasi nyingine ya majadiliano ya mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika na Nordic amesisitiza juu ya umoja na umuhimu wa kushirikiana katika  kukabiliana na changamoto za ulimwengu  kwa manufaa ya wote.

 

Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nchi za Nordic pamoja na mambo mengine umejadili masuala ya amani na usalama, migogoro, mabadiliko ya Tabianchi, masuala ya kimataifa, vijana na wanawake.

Mkutano wa 19 wa Mamwaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nordic umependekeza Algeria kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 20 wa Mawaziri hao unaotarajiwa kufanyika mwaka 2024.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Nordic baada ya kumalizika kwa mkutano wa 19 wa Mawaziri hao jijini Helsinki, Finland.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (kushoto) akifuatilia majadiliano katika mjadala wa vijana wa Nordic - Afrika amabo ulijikita katika namna ya kuwakwamua vijana kwa kuwapa ujuzi utakaowawezesha kujikwamua kiuchumi samabamba na kushirikikishwa katika masuala ya kijamii na taifa kwa ujumla.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Mhe. Pekka Haavisto ( kulia) akiongoza Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Finland uliofanyika tarehe 14 Juni 2022 jijini Helsinki, Finland.

Mkutano ukiendelea.

No comments:

Post a Comment

Pages