July 09, 2022

BATIKI YA TANZANIA SASA KUWEKEWA VIWANGO NA TBS

NA TATU MOHAMED 

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amesema katika stadi za ujasiriamali Vazi la Batiki litawekewa viwango ili mtu yeyote duniani akishika vazi hilo litambulike kuwa ni Batiki kutoka Tanzania.


Waziri Gwajima ametoa kauli hiyo wakati wa Siku ya vazi la Batiki ambayo imefanyika kwenye Viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam wakati wa Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea. 

"Tunataka mahali popote vazi hili la Batiki mtu akilishika ijulikane kuwa ni Batiki ya Tanzania kwani ni kwa njia hiyo tutaweza kuwakomboa watu wetu na Umasikini" amesema Dkt. Gwajima.

Ameongeza luwa  lengo ni kuwafikia watengenezaji wa Batiki  wakiwemo Wanawake walio wengi kwenye Sekta ya Biashara ndogo ndogo ili kila mmoja aweze kuinuka kiuchumi.

Dkt. Gwajima amesema kuwa, Rais Samia Suluhu Hassan amefungua fursa kwa Wanawake na kuwaonesha kuwa wanaweza, hivyo nimuhimu kuchapa kazi kwa kushirikiana na Wanaume kuinua Uchumi wa Nchi.

"Kutungwa kwa Sheria ya Fedha za Mamlaka za Serikali za Mitaa ya mwaka 2018 inayozitaka Halmashauri zote kutenga 10% ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo isiyo na riba kwa makundi maalum ikiwemo wanawake imewasaidia wengi ambapoMwaka 2020/21 zilitengwa jumla ya Sh. Bil. 62.68 na kufikia 30th Juni, 2021 Sh. Bil. 53.81 zilikopeshwa kwa Vikundi 7,993 vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu sawa na asilimia 86" alisema Dkt. Gwajima.

Amebainisha kuwa, kati ya Fedha hizo Sh. Bil. 28.17 zilitolewa kwa vikundi vya wanawake 4,894 vilivyozalisha ajira 52,428.

Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Mhe. Riziki Pembe amewahimiza waandaaji wa Siku ya Batiki kufanyika nchi nzima. 

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Zainab Chaula ameahidi kushirikiana na Katibu Mkuu wa Zanzibar kufanyia kazi maelekezo ya Mawaziri hao.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara TanzaniaBi. Latifa Mohamed Khamis, aliomba Serikali kuhakikisha Shirika la Viwango nchini TBS, wanatoa Vyeti vya Ubora wa Bidhaa za Batiki.

Awali Mkurugenzi wa Taasisi Roijok Progress Centre, Rose Urio amesema kuwa Uzinduzi huo ulikuwa na lengo la Kuitanga Batiki ndani na Nje ya Nchi.

Amesema uzinduzi huo utafungua Masoko ya Batiki pamoja na akuwaunganisha wazalishaji wa Batiki Tanzania kuwa na masoko ya ndani na nje ya Nchi.

"Tumefanya hii kwa msaada Mkubwa wa Serikali, tumekuwa na Viongozi wa Serikali ambao wamekuwa sababu kubwa ya sisi kufikia hapa.

Amesema kuwa Maisha yamebadilika thamani ya mwanamke ni kuweza kujitegemea kiuchumi ingawa Manamke anamajukumu makubwa ya kulea familia, lakini Mapinduzi Makubwa yaliyotokea dunia hivyo mwanamke anakila sababu ya kuingia kwenye uchumi.

Amesema Batiki ni bidhaa inayoweza kuzalishwa hata eneo dogo lenye uwazi. "Kwahiyo sisi Kama Roijok kupitia mradi wetu wa Batiki utasaidia kuanzia wazalishaji wadogo mpaka wenye Viwanda."

Amesema Lengo ni wanawake kuweza kuzalisha lakini pia kusimamia Familia.

Amesema katika Mradi wa Batiki wanampango wa kuzindua Ua la Mama ambalo litakuwa kwaajili ya Kumuenzi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassani.


No comments:

Post a Comment

Pages