July 15, 2022

Dk. Kijazi: Tumieni sheria ya Mamlaka kukusanya mapato

 

Dk. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), akizungumza na wafanyakazi wa mamlaka hiyo ofisi za Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA).

 

Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dk. Agnes Kijazi, ambaye pia ni Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) amewataka wafanyakazi katika ofisi za TMA zilizopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa  Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), kutumia sheria ya Mamlaka kukusanya mapato yatakayochangia uboreshaji wa huduma za hali ya hewa nchini.

Amesema hayo alipokuwa akifunga rasmi mafunzo ya siku nne yanayohusiana na uangazi wa anga la juu pamoja na taratibu za udhibiti wa ubora “Quality Management Systsem (QMS) procedures”, katika ofisi za TMA - JNIA.
 
“Ninasisitiza muda mrefu juu ya kufanya kazi kwa ushirikiano yaani “Team work” hali iliyotuwezesha kutufikisha mpaka tukapata sheria yetu ya Mamlaka, lakini sasa siongelei tena “Team work” kwani najua hiyo ipo tayari katika utendaji kazi wetu wa kila siku, lakini hivi sasa nazungumzia suala la mapato, tunatakiwa tuitumie sheria yetu ya Mamlaka vizuri katika ukusanyaji wa mapato yatakayochangia kuboresha zaidi huduma za hali ya hewa nchini”. Alisisitiza Dk. Kijazi.
 
Awali aliwapongeza wafanyakazi kwa kupata mafunzo hayo kwani yatawaongezea uelewa katika utendaji kazi wao wa kila siku sambamba na kupata nafasi ya kujikumbusha masuala ya QMS, kwa lengo la kuboresha huduma za hali ya hewa hususan kwa usalama wa usafiri wa anga.
 
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Meneja wa TMA, Kituo cha Hali ya Hewa JNIA John Mayunga, alimshukuru Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Kijazi na menejimenti yake kwa ujumla kwa kuwezesha kufanyika kwa mafunzo hayo muhimu ya siku nne, ambapo yalijumuisha kujifunza namna ya kutafsiri taarifa zinazotokana na uangazi wa anga za juu pamoja na namna ya kufanya kazi kwa kufuata taratibu za QMS.

Aidha, kwa upande wa wafanyakazi wa TMA wa JNIA walimpongeza Dk. Kijazi kwa utendajikazi wake mzuri kitaifa na kimataifa.

No comments:

Post a Comment

Pages