July 17, 2022

MAJALIWA: WATUMISHI ENDELEENI KUCHAPA KAZI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa umma nchini waendelee kufanyakazi kwa bidii, weledi na uaminifu kwa kuwa Serikali inaona na inaridhishwa na utendajikazi wao ikiwemo usimamizi wa miradi ya maendeleo ya wananchi inayotekelezwa katika maeneo yao.

 

“Tuna kazi kubwa ya kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020, ambayo yanatakiwa yatekelezwe kwa wakati, wakuu wa idara fanyeni marejeo katika kitabu hicho na mpanue wigo wa utekelezaji wa maelekezo hayo.”

 

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumamosi, Julai 16, 2022) wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba katika ukumbi wa halmashauri hiyo akiwa kwenye ziara yake ya kikazi mkoani Singida.

 

“Watumishi wenzangu tufanye kazi kwa kuzingatia uadilifu, uaminifu na wakati wote kila mmoja ahakikishe anajipanga vizuri katika sekta yake. Serikali inamatumaini makubwa na watumishi wa umma, hivyo mfanye kazi ambazo zitaleta matokeo chanya.”

 

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka watumishi hao wasitoe mianya ya wananchi kuwafuata maofisini na badala yake waweke utaratibu wa kuwafuata katika maeneo yao. “Nendeni vijijini wafuateni wananchi mkawahudumie huko huko, ofisini ni mahali pa uratibu, kazi zipo vijijini.”

 

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange amesema kuwa wamepokea magizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu na watahakikisha wanasimamia utekelezaji wake ili adhma ya kuwaletea ya Serikali wananchi maendeleo inafanikiwa.

Awali Mheshimiwa Majaliwa alikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa maji wa Ulemo-Misigiri unatekelezwa kwa fedha za Serikali kupitia mfuko wa maji wa Taifa kwa gharama ya shilingi milioni 569.3 na hadi sasa umefikia asilimia 94 ya utekelezaji.

 

Eeneo hili lina mito lakini tumeikausha kwa shughuli zetu za kibinadamu ikiwemo kupeleka mifugo, kukata miti na kulima pembezoni mwa vyanzo vya maji, leo hii tunatoa maji mbali kuyaleta Misigiri, Serikali za vijiji zina kamati za mazingira hakikisheni maeneo yote yenye vyanzo vya maji yanalindwa ili yabaki chepechepe”

 

Naye, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Singida Sebastian Warioba amesema kuwa awamu ya kwanza ya mradi huo ilihusisha uchimbaji wa visima vitatu vyenye uwezo wa kuzalisha lita 41,158 kwa saa.

 

Amesema kuwa shughuli zilizotekelezwa mpaka sasa ni Ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 400,000 umefikia asilimia 99, Ujenzi wa tanki la kabla(Sump tank) lenye ujazo wa lita 45,000 umefikia asilimia 96, Ujenzi wa vituo viwili ya kusukuma mitambo umefikia asilimia 100

 

Shughuli nyingine ni ununuzi na ufungaji wa miundombinu ya kuzalisha maji(lita 30,000 kwa saa na lita 17, 000 kwa saa) umefikia asilimia 100, Ununuzi na ulazaji wa mabomba ya kusafirisha maji yenye urefu wa mita 2,850 umefikia asilimia 99, Ununuzi na ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji yenye urefu wa mita 10,400 umefikia asilimia 100.

No comments:

Post a Comment

Pages