Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akizungumza na wananchi wakati wa ziara ya kusikiliza changamoto za wanyama wakali na waharibifu wa Kijiji cha Mkumbara, Wilaya ya Korogwe Vijijini Mkoani Tanga leo.
Na mwandishi Wetu
Serikali imejipanga kuja na mfumo maalum wa
kuwavisha tembo kola zijulikanazo kama visukuma mawimbi ili kutambua mwelekeo
wao kwa ajili ya kuwazuia kuingia katika makazi ya watu.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) katika ziara yake ya kusikiliza changamoto za
wanyama wakali na waharibifu iliyofanyika leo Kijiji cha Goha, Kwalukonge na
Kweisewa, Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga.
“Makundi ya tembo ambayo yanaonekana kuzagaa
tutayaingiza kwenye mtambo na tembo viongozi tutawafunga kola zijulikanazo kama
visukuma mawimbi na tutayafuatilia yameenda wapi.” Mhe. Masanja amesisitiza.
Amesema kupitia njia hiyo Askari wa Uhifadhi
wataweza kuwafuatilia kwa karibu na endapo kundi lolote la tembo litakuwa na
mwelekeo wa kuingia kwenye makazi ya watu, watalizuia kabla ya madhara kutokea.
Aidha, ameahidi kujenga kituo cha Askari wa
Uhifadhi katika vijiji hivyo ili kurahisisha zoezi la kuzuia uharibifu
unaofanywa na tembo.
Pia, amesema Serikali imejipanga kutoa elimu ya
namna ya kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu ambapo vijana
watafundishwa mbinu mbalimbali.
Kuhusu kifuta jasho/machozi ameahidi kuwa Serikali
itawalipa waathirika wote ifikapo mwezi wa nane mwaka huu.
Awali, mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Goha, Mohamed
Ramadhani amesema kuwa tembo wamekuwa wakivamia mashamba kila ifikapo saa 4
usiku na hivyo kuiomba Serikali kuwapeleka Askari wa Uhifadhi ili kuwa
kuwasaidia wananchi kukabiliana na adha hiyo.
“Inatakiwa kila Kijiji tuwe na watu wa TANAPA ili
tutoke nao kukabiliana natembo wakati wa usiku wanapokuwa mashambani na pia
watupe elimu yakukabiliana nao” amesema Bw. Ramadhani.
Naye, Mbunge wa Korogwe Vijijini, Mhe. Timotheo
Mnzava ameiomba Serikalikuangalia namna bora ya kuweka uzio ili kuzuia tembo ,
kujenga kituo cha askari wa wanyamapori na pia kuelimisha wananchi kuhusu mbinu
za kupambana natembo wanapovamia makazi yao.
Ziara hiyo ni mwendelezo wa ziara za kusikiliza
changamoto za wananchi nakuzipatia ufumbuzi.
No comments:
Post a Comment