August 06, 2022

Letshego, Assemble zashirikiana sekta ya bima

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Bima ya Assemble, Tabu Masoud akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), wakati wa hafla ya kusaini mkataba mauzo ya bidhaa za bima kati ya kampuni yake na Benki ya Letshego.
Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Letshego, Omar Msangi akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa mauzo ya bima kati ya benki yake na Kampuni ya Bima ya Assemble.

Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Letshego Omar Msangi (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Assemble Insurance Tabu Masoud, wakionesha mkataba waliosaini.


Na Irene Mark



SUALA la bima hasa kwenye afya linatakiwa kupewa kipaumbele na jamii ihamasike kupata bima ili kuwa na uhakika wa matibabu wakati wowote.

Kwa kuliona hilo na kuunga mkono juhudi za serikali, Kampuni ya Bima ya Assemble ikishirikiana na Benki ya Letshego, leo Agosti 5,2022 wamesaini mkataba utakaomuwezesha mwananchi kupata mkopo kwa ajili ya kukata bima za aina mbalimbali zinazotolewa na kampuni ya Bima ya Assemble.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za Benki ya Letshego jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Bima ya Assemble, Tabu Masoud alisema kupitia ushirikiano huo sasa bidhaa zote za bima za kampuni yake zitatolewa na benki hiyo ya Letshego.

"Tunaiunga mkono serikali kwa kupanua wigo wa huduma za bima, tunajua lengo la serikali ni kuhakikisha asilimia 90 ya watanzania wote wanakuwa na bima ya afya sisi tunawasogezea hudima za bima wananchi hivyo tunawahimiza kujikatia bima kwa kuwa maradhi hayapigi hodi.

“Sio afya tu, Assemble Insurance inatoa huduma zote za bima hivyo tunawakaribisha watanzania wakifika Letshego benki watapata huduma zote za bima zinazotolewa na Assemble bila kufika ofisini kwetu.

“Tunaunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita naamini lengo la sekta ya bima kuchangia asilimia 10 kwenye pato la taifa litafikiwa,” anasema Tabu.

Anataja bidhaa zitakazouzwa na  benki ya Letshego kwa mujibu wa mkataba huo kuwa ni bima ya afya, bima ya mali, bima ya moto na bidhaa mpya inayotolewa na kampuni ya Assemble iitwayo bima ya ustawi wa afya ya akili.

Mkurugenzi wa Benki ya Letshego, Omar Msangi anasema wamezindua ushirikiano utakaowezesha benki hiyo kuwa wakala wa kampuni ya Assemble.

Kwa sasa benki hiyo inatoa huduma ya mikopo nafuu na ya muda mfupi ya bima kuanzia miezi sita, nane hadi mwaka mmoja kulingana na matakwa ya mteja husika.

“Mkataba huu unaturuhusu sisi Letshego kumkopesha mteja kiasi cha fedha anachotaka kulingana na aina ya bima anayochukua hivyo atarejesha mkopo huo kwa bima ya asilimia ndogo kwa muda usiozidi mwaka mmoja,” anasema Msangi.

Anataja huduma nyingine zinazotolewa na benki hiyo kuwa ni akaunti ya wajasiriamali inayotoa riba nafuu kwa wafanyabiashara wadogo wanawake na akaunti ya mishahara inayolenga pia kutoa mikopo kwa watumishi wa umma.

Alisema pia wana huduma ya mkopo fasta kwa wajasiriamali wadogo na wanatoa mikopo inayofikia hadi Sh milioni 50.

"Ndoto yetu ni kuona hawa wajasiriamali wanaajiri watu 10 hadi 20 tukiwa nao sambasamba," alisema Msangi.

Benki ya Letshego ilianza shughuli zake hapa nchini tangu mwaka 2016 ikinunua hisa za asilimia 100 kutoka kwa benki ya Advance. Kwa sasa benki hiyo ina matawi nane nchi nzima yakiwemo matatu yaliyopo Dar es Salaam.

Matawi mengine yapo Mbeya, Arusha, Tanga, Dodoma, Mwanza, Manzese, Temeke na Kariakoo.


No comments:

Post a Comment

Pages