HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 28, 2022

Mongella apongeza UNDP kufadhili mradi wa uhifadhi Mwandishi Wetu, Arusha


 Mratibu wa Miradi Midogo wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Fastine Ninga akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa kutumia maarifa ya asili katika masuala ya uhifadhi ya mazingira.

Afisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Arusha, Blandina Mkini akizundua mradi wa uhifadhi mazingira ya asili kwa kutumia maarifa ya asili kwa niaba ya mkuu wa mkoa Arusha, John Mongela mradi ambao utatekelezwa katika wilaya tatu za mkoa wa Arusha.

 

MKUU wa Mkoa wa Arusha, John Mongella amezindua mradi wa uhifadhi wa mazingira kwa kutumia maarifa ya asili ambao  utatekelezwa na Shirika la Wanahabari la Usaidizi wa Jamii za Pembezoni (MAIPAC) na Shirika la CILAO. 

 

Mradi huo unahusisha Wilaya za Monduli, Longido na Ngorongoro  unafadhiliwa na Shirika la Msaada la Umoja wa Mataifa (UNDP), Mfuko wa Mazingira Duniani na  mashirika mengine ya kimataifa.

 

Akizungumza katika uzinduzi huo kwa niaba ya Mongella, Ofisa Maendeleo ya Jamii wa mkoa huo Blandina Mkini alipongeza  UNDP na mashirika mengine kuamua kutoa ufadhili  MAIPAC na CILAO, ili waweze kuendesha mradi huu ambao unatarajiwa kusaidia suala zima la utunzwaji wa mazingira nchini kwa kutumia maarifa ya asili.

 

“Nimeelezwa mradi huu, unalenga kukusanya taarifa njia za video na maandishi  za maarifa ya asili katika uhifadhi wa mazingira, utunzaji wa vyanzo vya maji, misitu  na  mabadiliko ya tabia nchi. Lakini pia kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira  katika wilaya hizi tatu,” alisema.

 

Mkini alisema  mradi huo umekuja wakati muafaka kwani  dunia inapita katika kipindi kigumu cha athari za mabadiliko ya tabianchi, ambayo yanatokana na uharibifu wa mazingira na matumizi makubwa ya nishati ambazo sio rafiki kwa mazingira.

 

“Kwa mara ya kwanza, naona mradi kama huu, utatekelezwa na  wanahabari, hili ni jambo jema kwani watasaidia sana kuelimisha jamii juu yetu kwa sababu wao ndio wamekuwa wakifanya jukumu hilo la kupasha habari,” alisema.

 

Alisema mradi huo, utakwenda kusaidia watungaji wa sera na wadau wengine, kuingiza maarifa ya asili katika mikakati ya kutunza mazingira badala ya kuamini jamii  hazina ujuzi wa asili wa kuhifadhi  wa mazingira.

 

Mkini alisema ofisi ya msajili msaidizi wamashirika yasiyo ya kiserikali mkoa Arusha, inapongeza kazi nzuri za MAIPAC na ipo tayari kutoa ushirikiano zaidi kuhakikisha mradi huo unafanikiwa.

 

Mratibu wa miradi midogo wa shirika la UNDP, Faustine Ninga alisema UNDP imetoa ufadhili katika mradi huo kwa kudhamini umuhimu wa maarifa ya asili katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.

 

“Sio kwamba hatuamini elimu ya kisayansi lakini tunataka elimu hizi mbili zifanye kazi pamoja kwa ufasaha zaidi, kwani kuna nchi zinafanya vizuri katika matumizi ya elimu ya asili katika uhifadhi wa mazingira,” alisema.

 

Alisema mradi huu utasaidia kurithisha maarifa ya asili kutoka kizazi kimoja hadi kingine baada ya kukusanya simulizi za  wazee katika uhifadhi wa mazingira na kuziweka katika mfumo rasmi.

 

“Tunaimani MAIPAC itatekeleza vizuri mradi huu ili kuvutia wadau wengine ambao wanataka kuendeleza miradi ya mazingira kwa jamii za pembezoni,” alisema.

 

Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma alisema mradi huo utakuwa na manufaa makubwa na unatarajia kushirikisha makundi ya wanawake, vijana na wazee katika wilaya hizo tatu za mkoa wa Arusha.

 

Juma alisema mradi huu utashirikisha vyombo vya habari katika kukusanya taarifa  na kutoa elimu juu ya maarifa ya asili ya masuala ya uhifadhi wa mazingira kwenye jamii za pembezoni.

 

Mkurugenzi wa CILAO, Odero Odero alisema katika mradi huo, wanatarajia  kwa jamii na watunga sera watakuwa na uelewa mpana juu ya  maarifa ya asili.

 

Ofisa Misitu  na Mazingira Wilaya ya Monduli Habibu Mwanga,  Ofisa Maendeleo ya Jamii Longido Grace Mgase  na  David Magembe Ofisa Misitu Ngorongoro, walieleza mradi huo utakuwa na umuhimu mkubwa katika jamii na kuahidi kushirikiana na MAIPAC na CILAO.

 

Mwanga alisema kwa wilaya ya Monduli, mradi utatekelezwa kata za Selela na Engaruka, huku Magembe alieleza mradi kutekelezwa msitu wa Engusero Sambu na Ngese ni katika maeneo vijiji vya Olbomba na Kimotowa.

No comments:

Post a Comment

Pages