August 12, 2022

Ocode yatekeleza kwa kishindo mradi wa 'bonga'kwa vijana ubungo

Mkurugenzi Mtendaji wa Organization for Community Development (OCODE), Joseph Jackson, akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na jinsi walivyojipanga katika miradi ya kuwasaidia vijana.

 

Na Victor Masangu
 

Katika kuwakomboa vijana  ambao wanashindwa kujiendeleza zaidi  pindi wanapomaliza masomo yao ya shule za msingi na sekondari Asasi isiyokuwa ya kiserikali ya ya Organization for Community Development (OCODE) imekuja na mpango wa mradi wa pili ujulikanao Kama Bongo lengo ikiwa ni kuwawezesha vijana.

Mradi huo ambao kwa Sasa unatekelezwa katika manispaa ya ubungoJijini Dar es Salaam  umeanzishwa maalumu kwa ajili ya kuweza kuwasaidia vijana wenye kuanzia umri wa miaka 13 hadi 19 ambao walishindwa kuendelea na mfumo rasmi wa elimu.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Ocode Joseph Jackson wakati wa halfa ya mahafali kwa vijana wapatao 193 ambao wameweza kuhitimu baada ya kumaliza masomo yao kutoka Veta na kufanikiwa kujifunza katika fani mbali mbali.

Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa lengo la mradi huo ni kuweka mipango madhubuti ambayo itaweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa vijana wa manispaa ya ubungo kuweza kupata fursa ya kujiajiri wao wenyewe na hatimaye kujikwamua kiuchumi.

"Katika mradi huu wa bongo tumejikita zaidi kwa vijana na kwamba una malengo makuu matatu ambayo moja wapo ni kuwapatia watoto fursa ya elimu Bora,lakini pili ni kuwapa vijana stadi mbali mbali za maisha na jambo lingine la tatu ni kuwasaidia vijana katika suala zima la kujikwamua kiuchumi ili wasiwe tegemezi,"alisema Jakson.

Aidha alibainisha kwamba mradi huo wa bonga kwa sasa ni awamu ya pili na kwamba vijana hao walioweza kuhitimu wataweza kuleta chachu ya mabadiliko kutokana na ujuzi na fani mbali mbali ambazo wamezisomea katika chuo Cha Veta.

Kwa upande wake mjumbe wa bodi ya Ocode Godfrey  Boniventura ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa bodi hiyo alibainisha kuwa kati ya wahitimu hao 193 waliomaliza wameweza kujifunza kozi tofauti ikiwemo ushonaji wa nguo.kupika.kupamba,fani ya kutengeneza simu,udereva pamoja na fani nyingine.

Aidha mjumbe huyo aliongeza kwamba katika fani hizo kwa kiasi kikubwa vinagusa maisha ya watu hivyo ana Imani kubwa vijana hao watakuwa mabalozi wazuri katika jamii kwa kile ambacho wamefundishwa na kuwasihi wasibweteke na badala yake waongeze ujuzi na ubunifu zaidi katika kutimiza malengo yao.

Katika hatua nyingine aliwataka kuachana na tabia ya kukaa katika makundi ambayo hayana msaada kwao na badala yake waweze kujiunga kwa pamoja kwa kuongeza thamani ya ujuzi wao ili waweze kupata soko kwa urahisi zaidi.

Naye Naibu Meya wa Manispaa ya Ubungo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo Hassan Mwasha ameipongeza Asasi ya Ocode kwa kuanzisha mradi huo wa kuwasaidia vijana na kuahidi kushirikiana nayo bega kwa bega kwa maslahi ya kuwakomboa vijana.

Pia aliwaasa vijana wote ambao wamebahatika kupata fursa ya mafunzo hayo kutokuwa na vitendo vya kuzagaa vijiweni na badala yake waweze kujiunga katika vikundi lengo ikiwa ni kupatiwa fursa ya mikopo ambayo itaweza kuwasaidia katika kupambana na wimbi la umasikini.

Naibu Meya huyo pia hakusita kuwakumbushia vijana hao kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika zoezi la sensa ya watu na makazi ambalo linatarajiwa kufanyika Agosti 23 mwaka huu kujitokeza kwa wingi ili serikali iweze kutambua idadi kamili ya wananchi wake.

Asasi ya Ocode imekuwa ikifanya kazi zake mbali mbali katika Manispaa ya Ubungo Jijini Dar es Salaam ambapo imekuwa ikitekeleza miradi ya elimu kwa vijana pamoja na kuboresha maisha ya jamii pamoja na sekta ya michezo.

 

No comments:

Post a Comment

Pages