August 12, 2022

Jeshi la Polisi Kanda Maalum latoa onyo wavunjivu wa amani Mechi ya Simba na Yanga

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum Dar es Salaam, ACP  Jumanne Muliro.

 

 Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam


Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limesema halitamvumilia mtu au kikundi cha watu kitachojihusisha na vitendo vya uvunjivu wa amani kuelekea Mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Simba na Yanga itakayochezwa Agosti 13 mwaka huu katika Uwanja wa Benjamini Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na wanahabari leo jijini humo Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum Dar es Salaam, ACP  Jumanne Muliro amesema jeshi hilo limejipanga vyema kuhakikisha kabla na baada ya mechi hali ya usalama na amani inatawala uwanjani hapo hivyo atakayebainika kwenda kinyume watamchukulia hatua za kisheria.

‘Usalama utaimarishwa kwa kiwango cha juu. Ni marufuku kwa mtu yeyote kwenda na silaha uwanjani isipokuwa vyombo vya dola vyenye jukumu la usalama eneo hilo. Tunawatoa hofu mashabiki watakaofika kushuhudia mchezo huo kuwa ulinzi ndani na nje ya uwanja utakuwa umeimarishwa kwa kiwango cha juu’amesema Kamanda Muliro.

Amesisitiza kuwa wamepiga marufuku kikundi au  mtu  yeyote kwenda na silaha uwanjani isipokuwa vyombo vya dola vyenye jukumu la usalama eneo hilo hivyo atayekiuka hawatasita kumchukulia hatua.

Ameongeza kuwa kuwa hali ya usalama kwa Jiji la Dar es Salaam inazidi kuimarika kutokana na wananchi kuendelea kutoa taarifa mbalimbali za wahalifu,hivyo Polisi wamekuwa wakizingatia maadili, weledi na kuzitunza siri za wananchi.

Amewaomba wananchi kuendelea kuimarisha mifumo ya ulinzi shirikishi ikiwa ni pamoja na kutekeleza falsafa ya ulinzi shirikishii li kuzuia vitendo vya kihalifu.

Pia amesema jeshi hilo linaendelea na operasheni maalum kali ya kuzuia vitendo vya kihalifu maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam.



No comments:

Post a Comment

Pages