August 30, 2022

TAASISI YA JAKAYA MRISHO KIKWETE NA UNA-TANZANIA KUENDESHA MAFUNZO KWA VIJANA SEPTEMBA 2 NA 3 MAKUMBUSHO YA TAIFA (POSTA) DAR ES SALAAM


DAR ES SALAAM AGOSTI 30, 2022: Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete (JMKF) ikishirikiana na Asasi ya Umoja wa Mataifa  (UNA) Tanzania na wadau mbalimbali   itakutanisha Jumla ya vijana 150 katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kuimarisha biashara na kazi endelevu za mashirika ya Vijana mnamo tarehe 2 na 3 Septemba, 2022 katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa na Nyumba ya Utamaduni mtaa wa Shaaban Robert jijini Dar es salaam.

Mafunzo hayo, ambayo ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya Vijana duniani (IYD2022), yatakuwa jukwaa la kufichua fursa na rasilimali kwa vijana ambazo zitasababisha kukuza upatikanaji wa kazi zenye staha na kukuza ushiriki wao bora kwenye masuala yanayowahusu. Kitaifa maadhimisho haya yalifanyika tarehe 12 Agosti, 2022 kaulimbiu ikiwa “Kila Mmoja Anahusika Kujenga Uchumi Imara, Ustawi Na Maendeleo Endelevu: Jiandae Kuhesabiwa”

“Kutakuwa na mafunzo ya kusisimua kutoka kwa wataalam waliobobea katika sekta binafsi na asasi za kiraia. Mafunzo haya ambayo yameandaliwa kwa pamoja na vijana, yatatumika kuchochea ujuzi na maarifa, ushauri kutoka kwa wabobezi katika sekta husika ili  kuongoza mazungumzo baina ya vizazi. Maeneo ya mafunzo yaliyoainishwa katika programu yalipendekezwa na zaidi ya vijana 50 kutoka sekta binafsi na za kiraia”,anamasema Mtendaji Mkuu wa JMKF Bi. Vanessa Anyoti.

Bi. Anyoti anaongezea kwamba: “Siku ya Vijana Duniani imekua jukwaa muhimu la kuthamini mchango mkubwa  wa vijana katika kuleta maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.  Tanzania inaungana na mataifa mengine Wanachama wa Umoja wa Mataifa kujadili, kusherehekea na kutambua nafasi ya Vijana katika kuleta maendeleo ya kiuchumi, kutoa mapendekezo na kuonesha uwezo wa vijana.  

Hii, inatokana na ukweli kwamba, vijana ndio kundi kubwa katika jamii yoyote ile. Vijana ndio wenye nguvu zaidi ya kufanya kazi, Vijana ni wabunifu, Vijana ndio chachu ya mabadiliko chanya katika jamii na Vijana ndio walinzi wa historia na warithi wa Mataifa yao”, anafafanua.

Kwa taarifa Zaidi wasiliana na Nicholaus Luoga kupitia 0759506122 na kupitia nicholaus.luoga@jmkfoundation.org

No comments:

Post a Comment

Pages