Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu (TET), Dk. Aneth Komba, akizungumza na waandishi wa habari.
Na Irene Mark
KIASI cha sh. bilioni 1.4 zimetumika kukusanya maoni ya wadau, kuchakata data na kuandaa rasimu za mitaala ya shule za awali, msingi, sekondari na vyuo vya ualimu kwa mwaka 2021/2022.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 9,2022 jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Aneth Komba anaeleza utekelezaji wa shughuli za Taasisi hiyo na mwelekeo wa mwaka 2022/2023.
Dk. Komba anasema sh. 1,427,030,000 zimetumika kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kufanya maboresho makubwa ya sita ya mitaala kwa maeneo tajwa.
Anaeema kazi ya kukusanya maoni hayo inafanyika Tanzania Bara na Zanzibar na kuyafikia makundi mbalimbali ya jamii kwa njia tofauti ikiwemo simu za mkononi, barua pepe, sanduku la barua, dodoso na tovuti ya TET.
“Katika kukusanya maoni, jumla ya wadau 103,210 wamefikiwa kupitia mikutano mikubwa mitatu iliyofanyika Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar.
“Tumwafikiwa wadau wa rika, kada na hali zote bila kuwasahau wamiliki wa shule, viongozi wa dini na wajumbe wa bodi za shule mbalimbali lengo ni kupata mtaala utakaogusa kila eneo ili kupata kilicho bora kwa elimu ya Tanzania na watoto wetu,” anasema Dk. Komba.
Akifafanua zaidia anasema kwa mwaka wa fedha 2022/2023 serikali imetenga sh. 1,769,340,000 kwaajili ya kukamilisha kazi ya maboresho makubwa ya mitaala ya elimu hapa nchini ambapo hadi Desemba 2022 Kamati ya kitaifa ya Mitaala ikishirikiana na TET itakuwa imekamilisha kazi hiyo.
Kuhusu uandishi wa vitabu vya kiada, viongozi vya mwalimu na vifaa vingine vya kutekeleza mitaala, mpaka sasa TET imekanisha kazi ya kuandika, kuchapa na kusambaza vitabu 28,469,667 vya shule za awali na msingi zinazotumia lugha ya kiswahili na kiingereza kufundishia na vitabu vya hadithi kwa uwiano wa wanafunzi wawili kwa kitabu kimoja.
“Upande wa wanafunzi wenye mahitaji maalum, TET imechapa na kusambaza jumla ya nakala 180,852 vya breli kwa wanafunzi wasioona wa darasa la kwanza hadi la saba na vimegawanywa kwa uwiano wa vitabu vitatu kwa mwanafunzi mmoja.
“TET pia imechapa na kusambaza nakala 155,562 vya maandishi yaliyokuzwa kwa wanafunzi wenye uoni hafifu kuanzia darasa la kwanza hadi la saba kwa uwiano wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja,” anasema Dk. Komba.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, vitabu vyote vimechapwa na kiwanda cha TET ambavyo ni Press A na B hivyo alichukua nafasi hiyo kuishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Awali alitaja kazi nne za TET ambazo ni kubuni, kuandaa na kuboresha mitaala kwa ngazi ya elimu ya awali, msingi, sekondari na elimu ya ualimu (astashahada na stqshahada).
Kazi nyingine ni kuandaa vifaa saidizi vya kutekeleza mitaala vikiwemo vitabu vya kiada, viongozi vya mwalimu, miongozo mbalimbali ya kufundishia na moduli pia kuidhinisha vitabu vya ziada.
Anataja kazi nyingine ya TET ni kutoa mafunzo kazini kwa walimu na wasimamizi wa utekelezaji wa mitaala (wathibiti ubora, maofisa elimu wa mikoa, wilaya na kata ili kuwawezesha kutekeleza mitaala kadiri ya matarajio.
Dk. Komba anasema TET pia inafanya utafiti na kutoa ushauri elekezi kwa serikali na wadau wengine wa elimu juu ya mitaala na masuala mengine yanayohusu ubora wa elimu hapa nchini.
No comments:
Post a Comment