Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi akizungumza wakati wa mkutano huo wa wadau uliofanyika leo Agosti 30,2022 jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Buruhani Nyenzi akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa mamlaka hiyo leo Agosti 30,2022.
Washiriki wa mkutano wa wadau wa Mamlaka ya Haki ya Hewa Tanzania (TMA), wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa mamlaka hiyo baada ya ufunguzi wa kikao cha wadau jijini Dar es Salaam leo Agosti 39,2022.
Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema imeendelea kupanua wigo wa utoaji taarifa za hali ya hewa kwa maeneo madogo madogo, ambapo msimu wa Vuli 2022 utaambatana na tabiri za wilaya zote 86 zilizo kwenye kanda za nyanda za juu kaskazini mashariki, pwani ya kaskazini na ukanda wa ziwa Viktoria.
Hayo yalizungumzwa na Mwenyekeiti wa Bodi ya TMA Dk. Buruhani Nyenzi wakati akifungua rasmi Mkutano wa Wadau wa Utabiri wa Mvua za Vuli 2022 katika Ukumbi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Dar es Salaam, Tarehe 30/08/2022.
“Utabiri huu wa msimu wa Vuli utaambatana na tabiri za wilaya zote themanini na sita (86) zilizomo kwenye kanda za nyanda za juu kaskazini mashariki, pwani ya kaskazini na ukanda wa Ziwa Viktoria. Hivyo, mimi binafsi napenda kutoa pongezi nyingi sana kwa hatua hii kubwa ya kuongeza wigo wa utoaji wa utabiri wa hali ya hewa hususan kwa watumiaji wa taarifa za hali ya hewa wa sekta na maeneo mbalimbali ambao wamekuwa na uhitaji wa taarifa hizi kwenye maeneo yao,” alisema Dk. Nyenzi.
Alisisitiza ushirikiano katika kuhakikisha kwamba taarifa hizo zinawafikia watumiaji wa mwisho kwenye sekta mbalimbali ili kuweza kuchangia katika ukuaji wa uchumi na kuleta tija pamoja na kufuatilia kwa karibu, kuelewa, kupanga na kukabiliana na hali ya hewa inayotarajiwa katika sekta zao.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani, Dk. Agnes Kijazi alieleza kuwa kauli mbiu ya mkutano wa mwaka huu ni “Matumizi Sahihi ya Taarifa za Hali ya Hewa kwa Maendeleo Endelevu” hivyo, katika kuendana na kaulimbiu hiyo, TMA imeendelea kuboresha taarifa zake kwa kutoa utabiri mahususi kwa sekta mbalimbali na kuongeza thamani katika taarifa zake za utabiri wa msimu kwa kujumuisha taarifa za maeneo madogo madogo kwa ngazi ya wilaya.
“Wakati Serikali ya awamu ya sita ikiendelea na jitihada za kukuza uchumi wa nchi pamoja na kuboresha miundombinu na huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo huduma za hali ya hewa, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaendelea kuweka msisitizo wa matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa kwa kila sekta ili kuongeza tija katika uzalishaji”.Alizungumza Dkt. Kijazi.
Kwa upande wa mdau kutoka Wizara ya Kilimo, akizungumzia utabiri wa msimu uliopitaBw. Juma Makandi alisema mara baada ya kupata taarifa za utabiri wa msimu wa mvua za Masika za awali na zilizohuishwa, wizara iliaandaa tafsiri ya utabiri huo katika uzalishaji wa mazao ya chakula na kuwasilisha kwa wadau mbalimbali kwa utekelezaji wake.
Katika Mkutano huo, wadau walipata fursa ya kuona rasimu ya utabiri wa hali ya hewa katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba 2022 na kuweza kutoa ushauri utaowezesha kuandaa mbinu na mipango ya kukabiliana na athari (hasi au chanya) za utabiri huo. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inatarajia kutoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za Vuli 2022 kupitia vyombo vya habari Septemba Mosi, 2022.
No comments:
Post a Comment