Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (wa tatu kulia) na Mwenyekiti wa Bunge SC, Abbas Tarimba, wakionesha baadhi ya jezi zilizotolewa na NMB kwa ajili ya timu za Bunge za michezo mbalimbali. NMB imezikabidhi timu hizo vifaa vya michezo vyenye thamani ya Sh. Mil.20, vitakavyotumiwa katika Bonanza la NMB Kivumbi na Jasho 2022, litakalofanyika Jumamosi Septemba 17 kwenye viwanja vya Chinangali Park na Kilimani jijini Dodoma. Wengine ni manahodha wa timu za michezo mbalimbali.
Na Mwandishi Wetu
MSIMU wa pili wa Tamasha la ‘NMB Kivumbi na Jasho,’ linalokutanisha timu za michezo mbalimbali za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya NMB, utaunguruma kesho jijini Dodoma, hii ni baada ya leo benki hiyo kuikabidhi Bunge SC vifaa vya michezo vyenye thamani ya Sh. Milioni 20.
Kivumbi na Jasho ni bonanza linalolenga kujenga na kuimarisha mahusiano mema baina ya Bunge na NMB, ambapo Bunge SC imeahidi kulitumia vema kama ilivyofanya msimu uliopita, ili kuzipa makali timu zao zinazojiandaa na Mashimdano ya Mabunge kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA 2022).
Akizungumza wakati akipokea msaada wa vifaa hivyo, Mwenyekiti wa Bunge SC, Tarimba Abbas, alisema wanalichukulia kwa uzito mkubwa tukio la leo, na kuwa kwao Kivumbi na Jasho ni zaidi ya bonanza, na wanalipa hadhi ya mashimdano, kwani limekuwa msaada katika maandalizi yao ya EALA 2022.
"Tunatambua na kuthamini malengo ya bonanza hili, lakini tuwe wazi kwamba kwetu ni zaidi ya hapo. Mwaka Jana lilitupa kipimo sahihi kuelekea EALA 2021, ambako tuliibuka washindi wa jumla katika michezo nane tuliyoshiriki. Tunatarajia kurejea mafanikio hayo mwaka huu kupitia bonanza hili," alisema.
Tarimba ambaye pia ni Mbunge wa Kinondoni, Dar es Salaam, alieleza kuwa wabunge, wafanyakazi NMB na waalikwa watakaohudhuria hafla ya usiku baada ya bonanza watapata fursa ya kuangalia 'live' kupitia televisheni kubwa mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF CC 2022/23), kati ya Yanga na Zalan FC ya Sudan Kusini.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, awali aliushukuru uongozi wa Bunge SC na manahodha wa timu za michezo yote, kwa kuipa nafasi NMB ya kuendelea na msimu wa pili wa bonanza hilo, ambalo hubeba fursa mbalimbali sio tu kwa Bunge, bali taasisi zingine za Serikali.
“Bonanza litaanza saa 12 asubuhi kwa matembezi yatakayoanzia Viwanja vya Bunge hadi Chinangali Park itakochezwa michezo mbalimbali, kuthibitisha faida za bonanza hili, tukifika pale tutakabidhi vifaa kwa ajili ya Hospitali ya Uhuru, vyenye thamani ya Sh. Mil. 50 na baada ya hapo, ndipo Kivumbi na Jasho kitakapoanza.
“Program hii ya Kivumbi na Jasho tuliianzisha mwaka jana, na tuwahakikishie wabunge kwamba bonanza hili litakuwa endelevu, na hii yote ni katika kuhakikisha kwamba tunaendeleza mashirikiano mazuri yaliyopo baina yetu na Wabunge, Ofisi ya Bunge na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.
Zaipuna alibainisha kwamba michezo ni afya, ni biashara, ni ajira. Lakini pia ni kazi na kwamba ushiriki wa wabunge - ambao ni wawakilishi wa wananchi, unatoa na kuakisi taswira ya umuhimu wa michezo kwa taifa na vijana kwa ujumla, huku akiwakaribisha wakazi wa Dodoma kuhudhuria bonanza hilo.
Vifaa vilivyokabidhiwa kwa timu za Bunge ni pamoja na ‘track suit’ maalum na jezi za soka, netiboli, wavu, kikapu. Baadhi ya michezo itakayoshindaniwa, ni mpira wa miguu, mikono, kikapu, wavu, kuvuta kamba, kukimbiza kuku, mbio za magunia, mbio fupi na mingineyo, ambapo washindi watakabidhiwa vikombe na medali
No comments:
Post a Comment