HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 09, 2022

TALGWU yaiomba Serikali kufanya Mabadiliko Tozo za Kibenki na Simu kuwapunguzia mizigo Watumishi wa Umma


Mkuu wa Idara ya Habari na Uhusiano wa Kimataifa wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) Shani Kibwasali akizungumza na wanahabari Jijini Dar es Salaam.

 

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam


Serikali imeombwa kufanya Mabadiliko katika Sheria ya Tozo za Miamala ya Kibenki na Simu ili kuepuka malipo ya mara mbili kwenye mishahara wa watumishi wa umma. 

Ombi hilo limetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Idara ya Habari na Uhusiano wa Kimataifa wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) Shani Kibwasali wakati akizungumza na wanahabari kuhusu Taarifa ya Utekelezaji wa Shughuli za chama hicho kwa kipindi cha Mwezi Januari hadi Juni 2022.

Amesema kuwa tozo hizo zinawabebesha mizigo na kuwakandamiza wafanyakazi huku ikizingatiwa mishahara wanayopata haikidhi mahitaji ya kila siku na familia zao. 

“Pia naomba nizungumzie suala la tozo za kibenki lililoanza kutekelezwa hivi karibuni. Tozo hizi zinawaathiri sana wanachama Wetu. Ikumbukwe kwamba watumishi wa umma kila mwezi wanalipa Kodi kwa kukatwa katika mishahara yao,” amesema Kibwasali na kuongeza kwamba,

“Lakini sasa kuanza kuanza kutekelezwa kwa tozo ya Serikali kwa miamala ya kutoa na kuhamisha fedha katika benki inamfanya mtumishi wa umma kutozwa zaidi ya mara mbili katika Pato moja kwa mwezi,”.

Amebainisha kuwa kuhusu suala la nyongeza ya mishahara,  ni ukweli usiofichika kwamba wanachama wao ambao ni wahanga wakubwa kwani bado wanamanung’uniko na TALGWU kama msemaji wao hawajaridhika kabisa kwa jinsi nyongeza ya mshahara ilivyofanyika.

“Ila naomba niwatoe hofu wanachama wetu kwamba suala hili linashughulikiwa na Chama kwa kushirikiana na shirikisho la vyama huru vya Wafanyakazi nchini (TUCTA),” amesema Kibwasali.

Katika hatua nyingine,  kuhusu mafanikio ya TALGWU kwa kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu, amesema hadi kufikia Juni 2022 walikuwa na jumla ya kesi 140 ambapo mawakili wa chama wanasimamia kesi 100, mawakili wa nje wanasimamia kesi 13, na rufaa zilizopo Tume ya Utumishi wa Umma ni 27.

Amesisitiza kuwa chama hicho kiliandaa utetezi kwa watumishi 12 waliokuwa wamepewa mashataka na waajiri. Hivyo amesema kati ya kesi 140 walizonazo zilizoisha zilikuwa ni 39 na chama kimeshinda jumla ya kesi 35 na kushindwa kesi nne huku kesi nyingine zikiendelea Mahakamani.

Amefafanua kuwa katika kipindi hicho TALGWU ilikuwa na jukumu jingine kubwa la kushughulikia haki na stahiki za wanachama ambazo kimsingi zipo kwa mujibu wa sheria ya Utumishi wa Umma na kanuni zake.

Hata hivyo, amesema TALGWU kinajivunia kuona Serikali imetekeleza maombi yao katika maeneo ya upandishaji vyeo na mishahara, malipo ya malimbikizo ya mishahara na Utawala Bora.

No comments:

Post a Comment

Pages