Na Benny Mwaipaja, Sirari, Tarime.
WAZIRI wa
Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu, amesema
kuwa Wizara ya Fedha na Mipango imepokea maelekezo ya Mheshimiwa Rais
Samia Suluhu Hassan na Chama cha Mapinduzi CCM kuhusu kushughulikia
malalamiko ya wananchi yaliyojitokeza kuhusu gharama za tozo za miamala
ya kielektroniki ili kuleta unafuu wa wananchi.
Dkt.
Nchemba alisema hayo kwa nyakati tofauti Wilayani Tarime mkoani Mara
alipofanya ziara ya kikazi ya kutembelea mpaka wa Tanzania na Kenya
katika mji wa Sirari na kuzungumza na wananchi, wafanyabiashara na
wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania -TRA.
Alisema
kuwa wataalam wa Wizara yake wanayafanyia kazi maelekezo mbalimbali
yaliyotolewa na Mhe. Rais, Chama Tawala pamoja na maoni ya wananchi
kuhusu jambo hilo na kuahidi kuwa muda si mrefu Serikali itakuja na
majawabu baada ya kufanya marekebisho kadhaa ili kuleta unafuu.
Dkt.
Nchemba alisema kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha ukusanyaji wa
mapato kwa ajili utekelezaji wa miradi ya maendeleo unaenda sambamba na
kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuweka miundombinu wezeshi inayolenga
kuibua wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa na hatimaye kuinua
kipato cha mwananchi mmoja mmoja.
“Serikali
imepokea maoni ya Watanzania wakati wa kutekeleza nia hii njema ya
Serikali kwa wananchi wake na kwa hiyo baada ya kupokea maelekezo ya
Mheshimiwa Rais kuhusu kuyazingatia maoni ya wananchi yanayoendelea
kutolewa, tunalifanyia kazi suala hilo na punde tutaleta majawabu”
Alisema Dkt. Nchemba huku akishangiliwa na wananchi wa Sirari
waliokusanyika kumsikiliza.
Alisema kuwa Serikali
inahitaji Fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati
pamoja na miradi mingine ya huduma za jamii ambayo pia inahitaji fedha
ndo maana kuna kugusana gusana kwa wale wenye unafuu ili kushiriki
kuchangia maendeleo hayo.
Aliitaja baadhi ya
miradi ambayo haiwezi kusimama kwa kukosa fedha ikiwemo ujenzi wa Bwawa
la kuzalisha umeme la Mwalimu Julius Nyerere unaogharimu zaidi ya
shilingi trilioni 6, Mradi wa Reli ya Kisasa-SGR unaogharimu zaidi ya
sh. trilioni 23, upanuzi wa bandari, miradi ya TARURA, ujenzi wa
hospitali na vituo vya afya, mradi wa elimu bila malipo, ujenzi wa
vyumba vya madarasa, mabweni na nyumba za walimu, na ujenzi wa vyuo vya
ufundi.
Aidha, alisema shughuli zingine muhimu
ambazo haziwezi kusimama ni ulipaji wa mishahara kwa watumishi,
kugharamia miradi ya kilimo ikiwemo utoaji ruzuku kwenye mbolea, utoaji
wa ruzuku ya mafuta ili kukabiliana na mfumko wa bei, na miradi mingine
inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini ambayo
inahitaji fedha nyingi.
Aliwasihi watanzania
kuendelea kuiunga mkono Serikali yao na kumwombea afya njema Mheshimiwa
Rais Samia Suluhu Hassan kwani ana nia njema ya kuharakisha maendeleo ya
wananchi na amefanya hivyo kwa vitendo katika kipindi kifupi
alichoshika madaraka ya nchi ambapo miradi mbalimbali ya kimkakati na ya
kijamii imetekelezwa kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea kabla yake.
Alitolea
mfano wa baadhi ya miradi inayokusudiwa kutumia fedha zitakazopatikana
kwenye tozo kuwa ni ujenzi wa vyumba vya madarasa vipatavyo elfu 17
kabla ya Januari, 2023 pamoja na ujenzi wa vyuo vya ufundi-VETA katika
wilaya 72 ambazo hazina vyuo hivyo ambapo jumla ya sh. bilioni 200
zitatumika kujenga vyuo hivyo.
Kuhusu mazingira ya
ufanyaji biashara katika mpaka wa Sirari na mkoa wa Mara kwa ujumla,
Dkt. Nchemba aliiagiza TRA kuhakikisha kuwa inafanyakazi yake ya
kukusanya kodi bila kuathiri biashara za wananchi na kuacha kutumia
mabavu kukusanya kodi hizo.
Aidha, aliwasihi
wananchi kushiriki katika maendeleo ya taifa lao kwa kulipa kodi kwa
hiari na kuwafichua wafanyabiashara wasio waaminifu wanaofanya magendo
na hivyo kuikosesha serikali mapato na hivyo kuathiri mwenendo wa uchumi
kwa kuleta ushindani usio sawa.
Aliahidi
kuzipitia na kuzifanyia marekebisho sheria mbalimbali za kodi
zinazokwaza ukuaji wa biashara nchini ili kuifanya sekta hiyo ya
biashara iweze kukua, kuzalisha ajira na kukuza uchumi wa nchi.
Kwa
upande wa wafanyabiashara, Dkt. Nchemba aliwataka kuacha kufanya
biashara za magendo mipakani kwani Serikali haiwezi kuhalalisha biashara
hiyo.
Awali wabunge wa Mkoa wa Mara, wakiwemo
Mbunge wa Tarime Vijijini Mhe. Mwita Waitara, Mbunge wa Viti Maalum mkoa
wa Mara Mhe. Ghati Chomete, Mbunge wa Tarime Mjini Mhe. Michael Kembaki
na Mbunge wa Jimbo la Serengeti Mhe. Dkt. Jeremiah Amsabi,
waliwasilisha kero za wananchi wa mkoa wa Mara ikiwemo mahusiano duni
baina ya Askari, Uhamiaji na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA hali
waliyosema inakwaza ustawi wa wananchi na wafanyabiashara wa eneo hilo
hususan wanaoishi katika mpaka wa Tanzania na Kenya wa Sirari.
Miongoni
mwa changamoto hizo ni kukamatwa kwa wananchi wakiwa na bidhaa
wanazonunua nchini Kenya kwa bei nafuu ikilinganishwa na bei ya nyumbani
ikiwemo saruji, mabati, sukari, mbolea na baadhi ya bidhaa nyingine
ndogondogo ambazo wananchi wanazipata kutoka Kenya lakini wakiziingiza
Tanzania, hata kama ni bati kumi au mifuko miwili ya Saruji,
wanakamatwa.
Akiwa ameambatana na Kamishna wa
Idara ya Sera kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Elijah Mwandumbya,
Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alitembelea Kituo cha Forodha cha Pamoja
cha Sirari na kuzungumza na Wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania-TRA katika mpaka huo wa Tanzania na Kenya.
No comments:
Post a Comment