October 04, 2022

Mamlaka ya Masoko Ya Mitaji na Dhamana (CMSA), imezindua wiki ya uwekezaji duniani.

 


NA MWANDISHI WETU

Mamlaka ya Masoko Ya Mitaji na Dhamana (CMSA), imezindua wiki ya uwekezaji duniani.

CMSA kwa kushirikia na Taasisi ya Kimataifa inayohusika na Usimamizi na watoaji wa viwango vya Kimataifa vya masoko ya mitaji ulimwenguni  (IOSCO) inashiriki katika kuadhimisha wiki ya wawekezaji ulimwenguni iliyoanza Oktoba 3 mpaka Oktoba 7, 2022.

Afisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, CPA, Nicodemus Mkama, katika taarifa yake amesema lengo la kushiriki Wiki ya Wawekezaji Duniani ni kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa elimu kwa umma na ulinzi wa maslahi ya wawekezaji kwa kuangazia jitihada mbalimbali zinazofanywa na Mamlaka za usimamizi wa masoko ya mitaji katika maeneo haya muhimu.

"Wiki ya Wawekezaji Ulimwenguni inahusisha Mamlaka za usimamizi wa masoko ya mitaji ambazo ziko chini ya IOSCO pamoja na wanachama wengine wa IOSCO katika mabara sita ambazo hufanya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na uzinduzi wa njia za mawasiliano na huduma zinazomlenga mteja, kukuza ushindani wenye tija unaolenga kuongeza wigo wa mikakati mbalimbali ya utoaji wa elimu ya wawekezaji,"amesema.

Pia wataandaa warsha na makongamano, pamoja na kutumia Mamlaka zao kuendesha kampeni za kitaifa. 

Mkama amesema Wiki ya wawekezaji inatoa nafasi ya upendeleo maalumu kwa wanachama wa IOSCO kufanya kazi kwa kushirikiana na wadau wote wanaotoa elimu ya uwekezaji kwa umma kwa ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

 Kauli mbiu ya mwaka huu ni uhimilivu wa wawekezaji na Mitaji Endelevu.

Mkama amesema Wiki ya Wawekezaji Ulimwenguni inatarajiwa kuongeza uelewa wa fursa na faida za kutumia masoko ya mitaji nchini ambao unalenga “ Kutambua Ushindani na Maendeleo ya Viwanda kwa Maendeleo ya Watu”. 

Pia inalenga kuongeza ushiriki wa wawekezaji katika masoko ya mitaji hivyo kuwezesha utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha na Mpango Mkuu wa Taifa wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha.
Aidha amesema wiki ya Wawekezaji Ulimwenguni imeambatana na maono ya Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi uliotukuka wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambao unalenga kuweka mazingira wezeshi kwa maendeleo ya sekta ya fedha kwa kuchochea maendeleo na ukuaji wa uchumi Nchini.

Katika kuadhimisha wiki hii, CMSA itafanya shughuli mbalimbali zinazolenga kuongeza uelewa, upatikanaji, ushiriki na kulinda maslahi ya mwekezaji katika masoko ya mitaji kuanzia tarehe 3 mpaka 7 Oktoba 2022. 

Programu hii inalenga kuimarisha uelewa kuhusu masoko ya mitaji hivyo kuchangia kwenye ajenda ya Taifa ya kuboresha Huduma Jumuishi za kifedha na maendeleo ya uchumi.
Mwisho

No comments:

Post a Comment

Pages