October 03, 2022

CRDB yazindua rasmi Wiki ya Huduma kwa Wateja Dar, wateja wafurahia huduma zake

Wakati makampuni na taasisi dunia nzima zikiadhimisha ‘Wiki ya Huduma kwa Wateja’ mwaka 2022, Benki ya CRDB imeianza wiki hiyo kwa kuwashukuru wateja wake kwa maoni na ushauri ambao umeiwezesha benki hiyo kutoa huduma bora na zenye viwango vya kimataifa kwa jamii.


Salamu hizo za shukrani zimetolewa na Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo wakati wa hafla iliyofanyika katika tawi la Benki hiyo lililopo Oysterbay, Jijini Dar es Salaam. Nshekanabo alisema wateja wamekuwa msingi mkubwa kwa Benki ya CRDB kufikia mafanikio ambayo imekuwa ikiyapata kufikia kuwa ‘Benki Bora zaidi Tanzania’.
 
 “Tukiongozwa na kaulimbiu yetu ya ‘Benki inayomsikiliza mteja’ tumekuwa tukipokea maoni na ushauri wa wateja ambao kwa kiasi kikubwa umechangia ubora wa huduma na bidhaa zinazotolewa na benki yetu. Hii inaonyesha ni kwanamna gani mteja amepewa kipaumbele kikubwa katika mkakati wa biashara yetu,” aliongezea Nshekanabo.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja Benki ya CRDB, Yolanda Uriyo amesema pamoja na kuwashukuru wateja, katika Wiki ya Huduma kwa Wateja mwaka huu wamedhamiria kuwasherekea wale wote walio mstari wa mbele kuiwezesha benki hiyo kutoa huduma bora”.

“Wakati dunia nzima ikiadhimisha wiki hii kwa kaulimbiu ya ‘Celebrate Service’ inayomaanisha kusherehekea huduma, kwetu sisi hii ni zaidi ya kaulimbiu kwani mafanikio tuliyonayo yanatulazimisha kuwasherehekea wanaotufanya tuwe bora zaidi; wateja na wafanyakazi wetu,” alifafanua Uriyo.

Uriyo alisema Benki ya CRDB itaitumia wiki hii kuwashkuru na kuwasherehekea wateja ambao wamekuwa chachu ya huduma bora zinazotolewa na benki hiyo. Aidha, watakuwa wakiwasherekea wafanyakazi ambao wamekuwa wakitoa huduma bora kwa weledi na ubunifu mkubwa.

Benki ya CRDB inatajwa kuwa benki inayoongoza kwa huduma bora kwa wateja. Mwaka huu benki hiyo imetunukiwa tuzo ya ‘Benki Bora Tanzania’ na jarida maarufu duniani la nchini Uingereza la Euromoney. Mwaka jana mwishoni benki hiyo ilitunukiwa ‘Tuzo ya Ubora’ na Taasisi ya Utafiti wa Ubora barani Ulaya (European Society for Quality Research).
 
Katika miaka ya hivi karibuni Benki ya CRDB imeweka kipaumbele na kufanya uwekezaji mkubwa katika huduma kwa wateja. Benki hiyo imewekeza katika mifumo ya kisasa na ya kidijitali ya utoaji huduma, ikiwamo mifumo ya mawasiliano, ambayo imesaidia kuongeza ufanisi katika matawi yake zaidi ya 260 yaliyosambaa kote nchini.

Uwekezaji huu pia umeongeza ufanisi katika njia mbadala za utoaji huduma; CRDB Wakala zaidi ya 22,000, ATMs zaidi ya 550, na huduma za SimBanking, SimAccount, na Internet banking. “Benki pia imewekeza katika mafunzo kwa wafanyakazi ili kuwawezesha kupata weledi pindi wanapowahudumia wateja. Hii imeenda sambamba na uboreshaji wa taratibu zetu za utoaji huduma (processes) ili ziendane na mahitaji ya wateja,” alisema Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo.
 

 

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe, akizungumza katika hafla ya ufunguzi rasmi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja yenye kauli mbiu "Sherehekea Huduma" iliyofanyika leo kwenye Tawi la Benki ya CRDB, Oysterbay, jijini Dar es Salaam.

 

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni (wa pili kulia) akikabidhi zawadi  mmoja wa wateja wa benki ya CRDB, Dk. Redempta Mbatia (kushoto) wakati wa hafla ya ufunguzi rasmi wa wiki ya huduma kwa wateja yenye kauli mbiu 'Sherehe Huduma'  iliyofanyika leo katika Tawi la Ostabey Masaki jijini Dar es Salaam (wa pili kushoto ni Afisa Mkuu wa Fedha Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo na kulia ni Mkuu wa Kitengo Cha Huduma kwa Wateja wa benki ya CRDB, Yolanda Uriyo.

 
Afisa Mkuu wa Fedha Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo, akizungumza na wateja wa benki hiyo katika hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja iliyofanyika katika Tawi la Oyster bay Masaki jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Kitengo Cha Huduma kwa Wateja wa benki ya CRDB, Yolanda Uriyo, na wateja wa Benki ya CRDB wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja.

 
Baadhi wa Wateja wa Benki ya CRDB wakishiriki shidano fupi la kupamba Keki ikiwa ni sehemu ya kusherehekea ufunguzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja yenye kauli mbiu "Sherehekea Huduma" iliyofanyika leo kwenye Tawi la Benki ya CRDB, Oysterbay, jijini Dar es salaam.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe (wa pili kulia) akimkabidhi zawadi ya Shampeni Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Benki ya CRDB, Joseline Kamuhanda baada ya kushiriki shidano fupi la kupamba Keki ikiwa ni sehemu ya kusherehekea ufunguzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja yenye kauli mbiu "Sherehekea Huduma" iliyofanyika leo kwenye Tawi la Benki ya CRDB, Oysterbay, jijini Dar es salaam. Wengine pichani ni Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo (wapili kushoto) pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja wa Benki ya CRDB, Yolanda Uriyo.
 
Sehemu ya wateja wa wafanyakazi wa Benki ya CRDB wakiwa kwenye hafla hiyo.


No comments:

Post a Comment

Pages