October 05, 2022

Miradi ya Maji Zanzbar kukabidhiwa Disemba

Na Salma Lusangi

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Nishati na Madini Mwanajuma Majid Abdullah amesema Wizara yake inatarajia kukabidhiwa miradi ya maji ifikapo Disemba mwaka huu, hivyo amewaomba wananchi wawe na subra kwani miradi hiyo imefikia asilimia 80 ya utekelezaji wake ikiwemo wa uchimbaji wa visima, ulazaji wa mabomba na ujenzi wa Matangi ya maji.

Akizungumza mara baada ya kushiriki ziara ya pamoja na kamati ya Ardhi, Mawasiliano na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar katika maeneo mbali mbali ya miradi hiyo. Alisema anafahumu kwamba tatizo la maji halistahamiliki lakini amewaomba wananchi kuendelea kupokea huduma ya maji kwa mgao kwani sio muda mrefu tatizo la maji litamalizika Zanzibar.

Alisema tatizo la maji Zanzibar limetokana na uwepo wa visima vichache ambavyo vinatumika pamoja na uchakavu wa miondombinu ya maji lakini kupitia jitihada za Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Mwinyi za kuwaondolea shida ya maji wananchi wake. Wizara ya Maji inaendelea kusimamia ipasavyo miradi hiyo ambapo ifikapo Januari, 2023 maji yatapatikana katika maeneo mengi ya Unguja na Pemba.

“Tumepiga hatua, tunamshukuru Mhe. Rais wa Zanzibar Dkt Mwinyi, miradi ya maji inayotekelezwa kwa fedha za Uviko 19, na fedha za Exim Bank ya India itakabidhiwa kwa Serikali Desemba, nimejionea mwenyewe ZAWA imefanya kazi kubwa, hivyo tatizo la uhaba wa maji litatatuka muda sio mrefu, naomba wananchi wamuunge mkono Mhe Rais  kwa kustahamili kidogo tu” Alisema. Mwanajuma”

Naye Mkurugenzi Idara ya Huduma za Maji Mudrik Fadhil Abas alisema kukamilika kwa miradi hiyo kusaidia maeneo mbali mbali ya wananchi kupata maji  kwasababu matangi ya maji yaliyojengwa hayapungui 300 kwa Unguja na Pemba hivyo asilimia kubwa ya wananchi watapata maji. Pia alisema na kila tangi limeshapangiwa maeneo ya kupeleka maji.

Alifahamisha kwamba mabomba ya maji yaliyolazawa kutoka kwenye kila tangi  yanaupana wa nchi 12 hali ambayo itasaidia kufikisha maji kwa haraka katika maeneo yaliyokusudiwa ili wananchi waweze kuendelea na shughuli zao za kiuchumi na kijamii na kusahau kabisa tatizo la maji Zanzibar.

Kwa upande wake Kaimu wa kamati ya Ardhi, Mawasiliano na Nishati ya Baraza la wawakilishi Zanzibar Kombo Mwinyi alisema ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maji, lakini amesisitiza kwamba miradi hiyo imalizwe kwa wakati unaotakiwa. Pia aliiagiza Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kuhakikisha kwamba wanawataalam wa wakutosha kwaajili ya kuendeleza usimamizi wa miradi hiyo.

Aidha alihoji changamoto ambazo zinaikabili (ZAWA) katika utekelezaji wa miradi hiyo kwa sababu hawapendi kusikia ifikikapo Mwezi Desemba miradi hiyo kuwa haijakamilika, kwani wananchi wamekabiliwa na tatizo la maji katika maeneo mengi ya Zanzibar.

Kwa Upande wake Mkurugunzi Mkuu ZAWA Mhandisi Dkt Salha Mohammed Kasim alisema changamoto ambazo zinamkabili ni uchelewaji wa vifaa kuingia nchini lakini changamoto kubwa inayomsumbua sana ni  ukosefu wa wataalamu hivyo ameiomba Serikali kuzingatia na kulifanyia kwani hata miradi ikikabidhiwa bado ZAWA inahitaji wataalamu kwasabau miradi inahitaji usimamizi wa hali ya juu.

Mwisho Mhandisi Dkt Salha aliihakikishie kamati hiyo kwamba ifikikao Desemba mwaka huu miradi ya maji itakabidhiwa, kutokana na hatua iliyofikiwa na juhudi zinazochukuliwa na taasisi yake.

Miradi ya Maji Zanzibar ikiwemo ujenzi wa matangi, ulazaji wa mabomba ,uchimbaji wa visima inatekelezwa kwa fedha za ahuweni Uviko 19 na  fedha za Exim Bank ya India na itawanufaisha wananchi wote wa Zanzibar.

 

No comments:

Post a Comment

Pages