October 06, 2022

ZAWA WASAKENI MAFUNDI WA MAJI MITAANI - KADUARA

 



Na Salma Lusangi


Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar Shaibu Hassan Kaduara ameagiza Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kuwatafuta na kuwachukulia hatua mafundi wa maji wa mitaani ambao wanaunga maji kwa wananchi kinyume na Sheria zilizoekwa na Wizara yake.


Akizungumza katika kikao na uongozi pamoja na wafanyakazi wa ZAWA huko Gombani, Pemba mwishoni mwa wiki aliwataka watendaji hao kuwatambua  wateja wao pamoja na kuwasaka mafundi wa maji wa mitaani ambao wanaunga maji kwa watu kinyume na Sheria.Alisema Wizara ya Maji, Nishati na Madini kupitia taasisi yake ZAWA imeshatoa muongozo kwamba watu wanaohitaji kuungiwa maji wafike katika ofisi hiyo kwaajili ya kujisajili.“ ZAWA hamuwajui wateja wenu, hamuwatambui mafundi wa mitaani! Mapato ya maji yanapotea kwasababu hamjawajibika ipasavyo. 


ZAWA watambueni wateja wenu, mafundi wa mitaani wanaowaungia watu maji kinyume na sheria ”. Alisema kaduaraPia alisisitiza umuhimu wa ZAWA kujipanga katika kukusanya mapato ya maji. Alisema endapo taasisi hiyo itajipanga vizuri katika ukusanyaji wa mapato basi wataweza kujilipa mishara mizuri sana na fedha zingine zitabakia.


 “Mkisimamia mapato vizuri basi mnaweza kujilipa mishara na pesa ya chenji zitabaki, simamieni mapato vizuri, kwani siku za nyuma makusanyo yalikua yanaenda vizuri, Mji wa Wete tu, mkisimamia vizuri basi mapato yataongezeka” Alielezea Kaduara.Aidha Waziri huyo alikemea tatizo la uwepo wa makundi ndani ya ofisi, ununuzi wa vifaa ambavyo sio sahihi kwa maana ya kutokua na vigezo vinavyotakiwa.


 Pamoja na kuwataka watendaji hao kusameheana endapo mtu amekwanzana na mtumishi mwenzake. Alisema kwani bila ya kusameheana watendaji hao hawataweza kufanya kazi kwa pamoja na kufikia malengo yaliyokusudiwa. 


Naye Katibu Mkuu wa wizara hiyo Joseph Kilangi aliwakumbusha watendaji hao nidhamu ya kazi, lugha nzuri kwa wateja  wao, umuhimu wa kusimamia matumizi sahihi ya fedha kwa kufuata mfumo uliyowekwa na Serikali, pamoja  na kuwahimiza kujibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) haraka.Pia aliwataka watendaji hao kuwa wabunifu wa kubuni miradi ya maendeleo ambayo italeta tija kwa Serikali na wananchi. Alielezea kwamba kuna baadhi ya Idara/Taasisi hazina miradi.


Aidha Katibu Mkuu huyo aliwataka mafundi wa ZAWA wasifunge mota za maji bila ya kushirikiana na wataalamu wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kwa sababu mota zinaungua, hivyo Serikali inapata hasara zaidi ya milioni mia tano.“Wizara yetu inamgusa kila mtu tujitahidi kuzuia malalamiko na kuzuia malalamiko hayo  ni kuwajibika, nidhamu, sisi tuliyopo ofisini tunatakiwa tutowe ripoti ya miaka miwili ya uongozi wa Rais Zanzibar Dkt Hussein kwa kuangalia ilani, hivyo timu iliyopo chini ya Afisa Mdhamini Pemba itekeleze wajibu wao” Alisema Kilangi.

No comments:

Post a Comment

Pages