MFANYAKAZI wa sasa ambaye ni mstaafu wa kesho, umepanga kufanya nini baada ya ukomo wako wa kuajiriwa ili kukuhakikishia uhakika wa mapato? Swali hili ni mihimu kwa kila mmoja kulitafakari, kwani ajira uliyonayo siyo ya milele bali ni wajibu wa kipindi kifupi tuu na baada ya muda huu wale walio kuajiri watakupa mkono wa kwaheri, huku kibindoni ukipewa furushi la fedha ambalo katu halina maisha marefu.
Baadhi ya watu wameshaanza kujipanga kwa kujihusisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi au hata kuwa na mpango maalum wa kujiwekea akiba ya ziada ya kifedha.

Mfano Rais mstaafu Dk. Jakaya Mrisho Kikwete alisema utakapofika wakati wa kustaafu kwake atakwenda kuendelea na kilimo cha mananasi na ufugaji wa ng’ombe kijijini kwake Msoga.
Tafiti za kisaikolojia zinaeleza kuwa wastaafu wengi hupoteza maisha muda mfupi baada ya kustaafu kwa kile kinachodaiwa kukata tamaa, ukata na kukabiliwa na msongo wa mawazo.
Hivyo ni vyema kuwa na nidhamu ya matumizi tunapokuwa katika ajira zetu au katika kujiajiri.
Hii itawezesha kutengeneza mtaji na kuanza kuweka vitega uchumi mbalimbali ambavyo vitatuhakikishia uhakika wa mapato hapo baadaye. Lakini ni jambo lililo dhahiri kuwa wengi hawafanyi hivyo ufikiapo umri ambao watu hulazimika kustaafu wengi wao uwezo wa kufanya kazi huwa umepungua.
Inakuwa ni aghalabu kuwa na uwezo wa kuhimili mikikimikiki ya hapa na pale hasa katika ufuatiliaji wa shughuli za ujasiriamali.
Bila ya shaka kwa wale walio katika mfumo rasmi hutegemea kupokea mafao na pensheni kuendesha maisha yao baada ya kustaafu.
Wengi wao hawana mpango mathubuti wa fedha hizo na katika kipindi kifupi hujikuta wamemaliza mafao na pensheni zao na kubaki katika hali ngumu ya kiuchumi.
Kwa kuliona hilo UTT AMIS taasisi ya serikali iliyo chini ya wizara ya fedha yenye jukumu la kuhamasisha jamii ya kitanzania kuwa na utamaduni na tabia ya kuweka akiba na kuwekeza kupitia mifuko ya uwekezaji wa pamoja ilianzisha Mfuko wa JIKIMU.
Mfuko wa JIKIMU ulianzishwa mwaka 2008. Mfuko huu wa uwekezaji wa pamoja una lengo la kutoa gawio la mara kwa mara huku ukilenga kukuza mtaji kwa wale wawekezaji wa muda mrefu.
Mfuko huu hauchagui bali unatoa fursa kwa Mtu, watu,Vikundi, kampuni za umma na binafsi, taasisi za serikali, SACCOS, mifuko ya hifadhi za jamii.
Mfuko huu una mipango miwili ya uwekezaji. Mpango wa gawio na mpango wa kukuza mtaji.
Mstaafu anaweza kunufaika na mfuko huu, ambao ni kwa ajili ya wote kama ilivyo elezwa hapo juu lakini leo mahsusi tumelenga kueleza jinsi mstaafu anavyoweza kunufaika kupitia mfuko huu.
Mpango wa gawio unaweza kumsaidia mstaafu kwa kumhakikishia uhakika wa kipato kila baada ya miezi mitatu au kwa mwaka mara moja.
Pamoja na uhakika wa gawio pia unampa fursa kukuza fedha zake hata baada ya kustaafu, pa kabla ya kustaafu anaweza akautumia mfuko huu kutengeneza mtaji wa maisha baada ya ukomo wa kazi.
Lengo ni kumhakikishia uhakika wa kipato kila baada ya muda wa miezi mitatu baada ya kustaafu- gawio mara 4 kwa mwaka.
Au mara moja kwa mwaka, chaguo ni la mstaafu mwenyewe kutokana na uwezo na malengo yake.
Mfuko hutoa gawio kila baada ya miezi mitatu au baada ya mwaka ili uweze kupata gawio kila baada ya miezi mitatu kiwango cha chini cha kuwekeza ni sh. 2,000,000 na kupata gawio kila mwaka kiwango cha chini cha kuwekeza ni sh. 1,000,000.Hakuna kiwango cha juu cha kuwekeza.
Kwenye mpango wa kukuza mtaji anaweza anza kuwekeza kwa sh. 5,000/= tu ili akuze mtaji na kufikia kiwango cha Sh. milioni 2 au 1 au zaidi na kuweza kuchagua kuingizwa kwenye mpango wa gawio endapo atapenda. Mpango huu unafaa zaidi uanzwe mapema kabla ya kustaafu, uwekezaji wa nyongeza baada ya uwekezaji wa awali unaruhusiwa hadi sasa mfuko una rasilimali ya zaidi ya sh. Bilioni 18.
Badala ya mtaafu kulipa tikiti au nyanya au hata kufunga kuku ambapo tunasema hatari za uwekezaji ni kubwa anaweza anza kukuza mtaji kupitia malengo ya muda wa kati na muda mrefu yaani kama miaka 5-10, mathalani akitengeneza mtaji kwa kuwekeza sh. 200,000 kila mwezi akapata sh. milioni 50 hivi kwa miaka kumi basi pesa hii itampa wastani wa sh. 500,000 kwa mwezi.
Sasa hii Sh. milioni 50 aliwekeza kidogo kidogo yeye aliwekeza kama shilingi milioni 24 tu akapata faida kuanza takribani sh. milioni 22 akachanganya na pension yake, fungu la jumla pengine ikawa hiyo hiyo milioni 50 ina maana atakuwa na milioni 100 ambayo itampa kama Sh. milioni 12 kwa mwaka ambayo kwa uchaguzi wake ataweza chukuwa Sh. milioni 3 kila miezi 3 Tangu kuanzishwa mfuko umekuwa ukitoa gawio na kuliboresha kila hali ya mfuko inaporuhusu.
Tulirudi kwenye mfano wetu wa mtaafu aliyekuwa na Sh. milioni 100 mwaka 2008 ina maana kila mwaka kapata wastani wa Sh. milioni 12 kwa miaka 13 ya fedha na leo hii pesa zake ziko sh. milioni 151. Hii ni zaidi ya upangishaji wa nyumba za kawaida. Hususan za nje ya kati kati ya jiji.
Vipande ni sehemu ya uwekezaji uliyonayo katika mfuko.Ikumbukwe kuwa bei ya vipande huweza kupanda na kushuka kutokana na hali ya soko.
Mathalani mstaafu aliyepata mafao ya sh. milioni 50, katika hali ya kawaida haitarajiwi aziwekeze fedha zote hizo katika shughuli zake za kijasiriamali kwa mkupuo.
Kama hamna mpango sahihi za matumizi ya fedha hizo zitaisha ndani ya muda mfupi na kumsababishia msongo wa mawazo, maradhi na hatimaye kifo cha mapema.
Mwekezaji ambaye amewekeza Sh. Milioni 40 wakati bei ya kipande ni sh. 151 atapata vipande na kwa gawio la sh. 3 kwa kila kipande atapa gawio la sh. 264,900 x 3 =sh. 794700 kila baada ya miezi mitatu.
Pamoja na gawio lakini fedha zake ziko salama na zinaendelea kuwekeza na kukua zaidi.
Sasa tukimtazama kwa upana mstaafu huyu tutatambua yafutayo; Anatarajia kupata fedha kutoka katika kitega uchumi ulichowekeza sh. milioni 10.
Pili anauhakika wa kupata pensheni yake kila baada ya mwezi au miezi mitatu sawa na utaratibu wa mfuko aliokuwa anachangia.
Tatu anauhakika wa kupata gawio kila baada ya miezi mitatu kutoka Mfuko wa Jikimu.
Kupanga ni kuchagua, Wanasema siku ya kwanza ya ajira ndo siku ya kwanza ya kuanza kupanga maisha yako baada ya ukomo wa kazi.
Na ukomo wa kazi ni mwanzo wa maisha mengine ya miaka 60 na kuendelea sio umri wa kujaribu maisha ni umri wa kufanya uwekezaji wenye hali hatarishi kidogo.
Pia tukiwa na miaka 60 nguvu za kuchacharika zina pungua, maradhi nayo yana nyemelea, misuli ina dhoofika na baadaye kumbukumbu zina anza kupotea basi tujipange ili maisha baada ya ukomo wa ajira rasmi yasiwe ya fedheha.
Chaguo ni lako karibu kwa wataalam wa uwekezaji, UTT, kwenye mabenki yetu, madalali wa masoko ya hisa ujifunze.
Pia tembelea Mamlaka ya masoko ya Mitaji na Dhamana Tanzania (CMSA) au hata Soko la Hisa Dar wa Salaam (DSE) ujifunze zaidi na uchukuwe hatua sasa.

No comments:
Post a Comment