November 03, 2022

Waziri Makamba: Bila ya kuwa na sera, sheria, kanuni na mifumo ya udhibiti hatuwezi kupata Nishati Safi ya Kupikia


Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

WAZIRI wa Nishati January Makamba amesema lengo la Mjadala kuhusu Sera, Sheria, Kanuni na Mifumo ya Udhibiti ya Kuwezesha Nishati Safi ya Kupikia ni kupata njia ya kufanikisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia nchini.

Makamba amebainisha hayo leo jijini Dar es Salaam katika Mjadala wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia kwenye mada iliyokuwa ikihusu Sera, Sheria, Kanuni na Mifumo ya Udhibiti ya kuwezesha nishati hiyo.

“Hili jambo hatuwezi kwenda kulifikia bila kuwa na Sera, Kanuni na Mifumo ya Udhibiti ya kuwezesha Nishati Safi ya Kupikia, Je ni mifumo ipi huwezesha upatikanaji wa Nishati Safi ya Kupikia,” amesema Makamba na kuongeza,

“Sasa kuna hatari ya mijadala hii kuwa na mitazamo tofauti ya kifalsafa na kiitikadi (sio ya kisiasa). Kikubwa ni kupata njia ya tunapotaka kwenda. Mwisho wa siku tunachotafuta ni njia na mkakati wa kufika tunapotaka kwenda,”.


Ametumia fursa hiyo kubainisha kuwa  moja ya kazi ya kikosi kazi kitakachoundwa ni kuja na njia na mkakati wa namna ya kufanikisha jambo hilo.

“Imani ni kwamba kikosi kazi kije na njia na mkakati wa kwenda tunapotaka kwenda (Kufikia Nishati Safi ya Kupikia),” amesisitiza Makamba.

Awali akichokoza mada hiyo Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine Prof. Romanus Ishengoma amesema Sera ya Nishati ya mwaka 2003 na 2015 zote zinalenga kuhama kwenda kwenye matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia. 

Hata hivyo Ishengoma amebainisha kwamba moja ya mapungufu ya Sera hiyo haitoi ufafanuzi kwamba Nishati Safi ya kupikia ni ipi na kwamba imeshindwa kutoa mwelekeo wa namna ya kufanikisha jambo hilo.

Hivyo ameshauri kwamba kama kuna uwezekano Sera hiyo ipitiwe upya au iungwe mkono kwa kanuni na sheria.

Vile vile ameshauri kwamba ili kufikia lengo la Nishati Safi ya Kupikia kwa kila mwananchi ni lazima kuwe na kipindi cha mpito kwani watu wa vijijini hawawezi kumudu gaharama kwa sasa kutokana na vipato vyao.

Katika hatua nyingine, amesema kuwa Serikali inawakaribisha wawekezaji wa bidhaa ya nishati kuja kuwekeza nchini ili kuchochea upatikanaji wa nishati safi na salama.

Pia amesema kuwa Serikali inaendelea kufanya jitihada za kuwakomboa wananchi wake waepukane na matumizi ya kuni ili kuwaepusha  na madhara ya kiafya yatokanayo na moshi.


No comments:

Post a Comment

Pages