Waandishi wa Habari Wanawake wakioneshwa maboresho yaliyofanywa katika Bandari ya Tanga.
Na Selemani Msuya
MAMLAKA
ya Bandari ya Tanga imesema maboresho ya bandari hiyo yatawezesha
kupokea zaidi ya tani milioni 3 za shehena za mizigo kwa mwaka, kutoka
tani 750,000, hali ambayo itachochea ukuaji wa uchumi wa nchi na
wananchi.
Hayo yamesemwa
na Meneja wa Bandari hiyo, Masoud Mrisha wakati akizungumza na waandishi
wa habari za uchumi, biashara na uwekezaji waliotembelea bandari hiyo
jana.
Mrisha amesema
Agosti 2019 Serikali iliagiza kufanyika kwa maboresho ya bandari hiyo
ambapo hadi yatakapokamilika Aprili 2023 jumla ya Sh.bilioni 429.1
zitatumika.
Amesema
maboresho ya bandari hiyo yatawezesha utoaji huduma kwa meli kubwa
ambazo awali zilikuwa hazifiki hapo, hivyo kusababisha gharama kubwa
"Zaidi
Sh.bilioni 429 zimetumika kufanya maboresho Bandari ya Tanga, matarajio
yetu ni baada ya kukamilika tutaweza kupokea mzigo mwingi hadi kufikia
tani milioni 3 kutoka tani laki 750,000," amesema.
Amesema
pamoja na kuongeza uwezo wa kupokea mzigo, pia mapato yataongezeka na
uchumi wa Tanga, mikoa ya Kaskazini na nchi kwa ujumla utakuwa.
Mrisha amesema pia maboresho hayo yatawezesha ajira kuongezeka.
“Gharama za Mradi huu kwa awamu ya kwanza ulikuwa Sh.bilioni 172.4,″ amesema Mrisha.
Mrisha
amesema maboresho hayo yamehusiha uongezaji wa kina cha maji kutoka
mita tatu hadi mita 13 na upana wa mita 73 kwenye njia ya kuingiza na
kutokea meli, ambapo awali mzigo ulikuwa unafutwa umbali wa kilomita 1.7
kutoka kwenye gati.
Meneja
huyo amesema kwa sasa wapo katika awamu ya pili ya maboresho ya bandari
ya Tanga yaliyoanza Septemba 2020 na hadi sasa yamefikia asilimia 83,
yanatarajiwa kukamilika Aprili 2023 ambapo takribani bilioni 256.8
zitatumika.
Amesema awamu hiyo ya pili ya mradi imehusisha maboresho ya magati mawili yenye urefu wa mita 450.
Mrisho
amesema maboresho, gati hizo mbili za Bandari ya Tanga zilizojengwa
mwaka 1914 na 1954, zimeongezwa kwa mita 50 upande wa Mashariki na mita
92 upande wa Magharibi kuelekea baaharini.
Mrisha amesema Bandari
ya Tanga ni fursa kwa wafanyabiashara wa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha
na Manyara pamoja na nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda, Zambia na
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
"Kuanzia
Aprili mwaka 2023 tutaanza kupokea meli kubwa mbili za mizigo na mbili
za mafuta hivyo tunawaomba Watanzania kutumia bandari hii, inafikika
kirahisi,"amesema.
Amesema
katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ongezeko la shehena katika
bandari ya Tanga limekuwa kwa wastani wa asilimia 20 kutoka shehena tani
502,426 mwaka 2017/18 hadi kufikia tani 986,308 mwaka 2021/22 kiwango
ambacho hakijawahi kufikiwa na bandari hiyo.
Meneja
huyo amesema Bandari ya Tanga imetoa ajira za moja kwa moja kwa
Watanzania 254 ambapo kati yao, 199 ni wanaume na wanawake ni 55 tu sawa
na asilimia 22.
Katika
mradi wa maboresho bandari ya Tanga pia inapanua wigo wa sehemu ya
kuhifadhia makontena kutoka uwezo wa kuhifadhi makontena 1,000 hadi
kufikia uwezo wa kuhifadhi makontena 12,000.
Ofisa
Masoko Bandari ya Tanga, Rose Tandiko amesema uli uwekezaji huo uwe na
tija katika mkoa na Tiafa, serikali inapaswa kushauri na kuelekezwa
wafanyabiashara wa mikoa ya karibu na bandari kutumia bandari hiyo.
"Huu
uwekezaji ni mkubwa sana, ili uwe na tija, tunaomba wawekezaji na
wasafirishaji hasa wa Ukanda wa Kaskazini kutumia bandari hii. Ni imani
yetu Serikali itaweka mkazo," amesema Tandiko.
Amesema mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na kwingineko inapaswa kutumia bandari hiyo kwani gharama zake sio kubwa.
Tandiko amesema mazao ya Kahawa, Mkonge na mengine yanapaswa kusafirishwa kupitia bandari ya Tanga.
Kwa
upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Pili Mnyema amewataka
wananchi wa Tanga na maeneo mengine kuwekeza Tanga ili waweze kunufaika
na bandari hiyo ya kisasa.
Mnyema
amesema faida zimeanza kuonekana katika mradi wa maboresho ya bandari
ya Tanga yanayoendelea kwani hivi sasa nchi jirani zimeanza kutumia
bandari hiyo.
“Faida
ambazo zimeanza kupatikana ni pamoja na nchi za Jumuiya ya Afrika
Mashariki ikiwemo Rwanda na Burundi kuanza kuitumia bandari yetu ya
Tanga kwa sababu inakuwa rahisi tofauti na sehemu nyingine” amesema
Mnyema.
Meya wa jiji la
Tanga Abdulrahman Shiloow amesema kukamilika kwa maboresho hayo yanaenda
kuleta mapinduzi ya kiuchumi mkoani humo.
Shiloow amesema ni wakati muafaka kwa wawekezaji kuwekeza Tanga, ili kuweza kuirejesha Tanga ya zamani.
"Tunamshukuru
Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu fedha za mradi huu, naamini
kilichobakia ni sisi wana Tanga na mikoa jirani kunufaika,"amesema.
Naye
Mwanahamis Msemo amesema maboresho hayo yamekuwa neema kwake, kwani
ameweza amepata kipato na kusomesha watoto wake na kupata mahitaji
mengine.
Amesema kupitia
kazi ambazo anafanya bandarini hapo, ameonesha wanawake wenzake kuwa
wanawake wanaweza na sio lazima wawe tegemezi.
“Nimepata kazi hii, imenisaidia mimi na familia yangu, nashukuru sana Bandari Tanga, wanawake tusichagu kazi," amesema.
No comments:
Post a Comment