HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 30, 2022

HAPPY NEW YEAR WANASIMBA

Na Mwandishi Wetu


Kheri ya Mwaka Mpya kwa mashabiki wa Simba na mashabiki wa Soka Tanzania. Unaweza kuelezea hivyo kwa kipigo kizito ambacho Simba SC wamewashushia Tanzania Prisons cha mabao (7-1) mchezo wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara NBC PL.



Mchezo huo umemalizika usiku huu Dimba la Benjamin Mkapa ikiwa ni raundi ya 19 mzunguko wa pili. Prisons wamekutana na kipigo hicho dhidi ya Simba ya Saido Ntibazonkiza akiwa anacheza mchezo wake wa kwanza akijiunga na wekundu hao wa Msimbazi akitokea Geita Gold FC.


Ni kama Prison waliingia kwenye mfumo wa Simba ya Clatous Chama na Saido Ntibazonkiza katika siku bora kazini, Pasi za Saido jumlisha mikimbio yake huku Chama akiwa anatokea pembeni mwa uwanja Prison walikosa kujua hatari ya Simba itatokea wapi?


Kivipi Chama na Ntibazonkiza walikuwa wanacheza kama double namba kumi huku wakibadilishana mikimbio ya kuiba nafasi katika eneo la hatari,  Prison walikosa uelewa wa mchezo na kujikuta wanapitika licha ya kuweka umbo la kiulinzi.


Pasi ya Saido kwa John Bocco anafunguka bao la kuongoza kabla ya makosa ya Aishi Manula kuwapa Prison kurejea mchezoni kwa kurejesha bao.


Samson Mbangula sijui alikuwa anawaza nini ni kama aliamua kuwatupia gunia la misumali wenzake akimchezea rafu mbaya Henock Inonga 'Baka' nankuoneshwa kadi nyekundu huku Inonga akishindwa kuendelea na mchezo.


Kipindi cha pili Simba walifanya kile ambacho mashabiki wao wakihitaji kwa kupora mipira mingi eneo la kiungo cha Prison ikawa ni kuwachapa tu bao baada ya bao na dakika 90 zinatamatika kwa Simba (7-1) Kheri ya Mwaka Mpya.


Mabao matatu ya Saido Ntibazonkiza na matatu ya John Bocco pamoja na Shomary Kapombe inakuwa salamu zaidi ya kuufunga mwaka na kuufungua mwaka huku pasi mbili za mabao kutoka kwa Chama zikisimika ushidi huo.

No comments:

Post a Comment

Pages