December 22, 2022

Mkataba TICS kufikia ukomo Desemba 31, 2022

 MAMLAKA ya Bandari Tanzania (TPA) imesema kuanzia Januari mwaka 2023, mkataba wa Kampuni ya Kimataifa ya Kuhudumia Shehena za Kontena Bandarini (TICS)  utakuwa umemalizika, hivyo Bandari itachukua eneo lake na kisha Serikali itaamua nani aendelee kutoa huduma zilizokuwa zinatolewa kwenye eneo hilo.


Aidha Mamlaka imesema pamoja na kwamba TICS haitakuwa ikitoa huduma wafanyakazi wote ambao walikuwa wanafanya kazi TICS ajira zao ziko pale pale na maslahi yao yataendelea kuwa salama huku ikitumia nafasi hiyo kueleza huduma ambazo zitakuwa zinatolewa zitakuwa bora zaidi ya ilivyo sasa

Akizungumza leo Desemba 21 mwaka huu Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Juma Kijavala  amesema ni vema ikafahamika mkataba wa TICS haujavunjwa bali umekwisha muda wake, hivyo TPA inachukua eneo hilo kwa ajili ya kuliendesha."Niwahakikishie huduma zetu zitakuwa bora kuliko ilivyokuwa awali."

Amefafanua kwa kutoa mfano wa mwenye nyumba anapoamua kumpangisha mpangaji ana hiyari kuamua aendelee na mpangaji wake baada ya mkataba kumaliza au laa, hivyo TICS amemaliza mkataba wake na hivyo eneo hilo litakuwa chini ya Bandari na Serikali itaaamua apewe nani kuliendeleza.

Pamoja na hayo ameeleza kuwa pamoja na TICS kuwa chini ya Bandari ajira za wafanyakazi wote ziko salama huku akisisitiza hata maslahi yao yako kama kawaida na wale walioko eneo la upakuaji na upakiaji mizigo wataendelea na majukumu yao.

No comments:

Post a Comment

Pages