HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 04, 2023

  AFANDE DIWANI KARIBU CHAMWINO


Adeladius Makwega-CHAWA

 

Januari 3, 2023 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amemteua Kamishna Diwani Athumani kuwa Katibu Mkuu Ikulu akiachana na majukumu yake ya awali.


 

Kwa wale wanaomkumbuka afande Diwani ni miongoni mwa Watanzania waliowahi kuonja machungu ya kutenguliwa, huku hilo la kutenguliwa kiongozi huyu siyo mada ya matini haya kwa leo.

 

Mwanakwetu mwenyezi Mungu kamjalia macho ya kuona vya karibu na vya mbali lakini vya ndani ya ukuta mweupe anaokwenda kufanya kazi ndugu Diwani mwanakwetu hawezi kuviona maana macho yake kila yakijaribu kutazama yanasharabiwa na miale ya mwanga kutoka katika rangi nyeupe iliyopakwa katika ukuta huu, hasa hasa katika msimu huu ya jua kali lakini mwanakwetu ana hakika afande Diwani hayo ya ndani atayakuta katika makabrasha ya nyumba hii nyeupe.

 

Mwanakwetu anampongeza sana afande huyu huku akimkaribisha Chamwino ilipo Ikulu kubwa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sasa ndugu yetu huyu anakwenda kusimamia shughuli kadhaa katika nyumba hiyo nyeupe yenye Ikulu kubwa mbili ile ya Magogoni na hii ya hapa kwetu Chamwino. Kwa ukarimu wa mwanakwetu kwa ndugu Diwani anaomba kwa hisani yake amkabidhi haya ya nje ambayo macho yake mwanakwetu yanayaona kila siku.

 

Ikulu hizi kubwa mbili zina tofauti kubwa za jamii zinazozunguka makazi na ofisi hiyo ya Rais. Ikulu ya Dar es Salaam inazungukwa na bahari na kwa kiasi kuna nyumba kadhaa za watu na ofisi za shughuli mbalimbali na binafsi na za umma, wakazi wake wengi ni wakipato cha kati na cha juu. Wakazi wa kipato cha chini ni wale wanaokwenda kupata huduma katika maeneo hayo jirani au wale wanaofanya kazi katika majengo hayo.

 

Ikulu ya Chamwino yenyewe inazungukwa na wanavijiji wengi mafukara wanaojishughulisha na kilimo cha jembe la mkono wakilima sana mahindi na nyumba zao za kawaida huku wachache mno wakiwa na nyumba bora zilizokamilika. Wakazi hawa wa asili wengi wao ni wale waliokuwa na ardhi na walilipwa malipo na kutoka ndani ya eneo ambalo sasa lina ukuta ndilo sehemu kubwa ya Ikulu ya Chamwino.

 

Mwanakwetu anaukodolea jicho uteuzi wa afande Diwani Athumani uende kujenga, kuimarisha mahusiano ya karibu na jamiii kando na nyumba hiyo nyeupe hasa hasa kwa Ikulu ya Chamwino.

 

Katika baadhi ya maeneo taasisi za umma zilizo kando na jamii zinajitahidi mno kutoa huduma kadhaa za kijamii ili kujenga udugu mathalani eneo la Mbalizi mkoani Mbeya kuna kambi ya JWTZ ambapo wakazi wa Mbalizi wanapata huduma za matibabu katika zahanati ndani ya kambi hilo. Kwetu Mbagala kuna kambi ya JWTZ ambapo nakumbuka hata ndugu zangu kadhaa wa damu waliweza kuolewa na wanajeshi waliokuwa wanafanya kazi na kambi hii. Hilo la Mbalizi na Mbagala limejenga udugu wa milele na wanajamii hizo.

 

Afande Diwani anapaswa kuwafahamu mno majirani wa Ikulu ya Chamwino katika mambo mengi, kwa mfano katika msimu huu wa kilimo wanavijiji wengi kando na eneo hilo wamepanda mahindi kwa kutumia mbegu za asili hawana uwezo wa kununua mbegu bora, kwa bahati nzuri mbegu hizo zote za asili zimeota vizuri lakini sasa ni siku ya sita mvua hakuna, hilo linaibua mashaka kwa majirani hao wa ukuta mweupe. Je vipi kama wangepanda mbegu bora? Hili ni jambo dogo sana ingeweza kutolewa mbegu bure kwa misimu miwili ya kilimo au angeagizwa Mkurugenzi Mtendaji wa eneo husika akatoa mbegu hizo kwa misimu miwili-Ndugu hawa wangeweza kuvuna mahindi mengi na wangepata chakula na wangejiongezea kipato.

 

Kwa ukweli wa Mungu ilitolewa ahadi kuwa msimu wa kilimo wa 2022/2023 kungetolewa bure mbegu bora ya mahindi lakini mpaka sasa haijaliwa kuwafikia wakulima hawa na ndiyo maana mbegu za asili zinapandwa na zimeota kama ilivyoelezwa.

 

Mungu bahati kwa sasa kuna mahindi yanayouzwa kwa bei pungufu yanapatikana katika ofisi ya Kijiji cha Chamwino hilo ni jambo zuri sana na pongezi kwa serikali yetu lakini ni heri kuingia gharama ya kutoa mbegu bure kwa wakulima wote kuliko kutoa mahindi ya kula maana haya yanakwenda kuliwa hayaendi kupandwa kwa maana kipandacho huota.

 

Afande Diwani hapa Chamwino wapo maafande wenzako wengi katika Kituo cha Polisi cha Chamwino wanachapa kazi kweli kweli na eneo mkabala na kituo hiki cha polisi lina mandhari zuri sana, yenye miti mingi kuliko eneo lolote lile. Afande ukifika msimu ya zambarau utakutana na mandhari ya rundo la watu kando ya kituo hicho hao mwanakwetu siyo waaharifu bali ni watu wanaokwenda kuokota na kuchuma zambarau za bure. Kipindi hicho wapo wanaoanguka, kuchubuka au kuvunjika viungo wakisaka zambarau za Chamwino. Hali ya njaa ikiwa kubwa hata umati wa wachuma zambarau unakuwa mkubwa zaidi.

 

Kwako afande Diwani, mwanakwetu anaiweka chini kalamu yake akisema AFANDE DIWANI KARIBU CHAMWINO ukutane na sisi wachuma zambarau.

 

makwadeladaius@gmail.com

 

0717649257

 

 

No comments:

Post a Comment

Pages