Akisoma mapendekezo ya mpango wa bajeti wa mwaka 2023/2024 kwenye kikao cha baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo katika ukumbi wa Halmashauri, Afisa Mipango wa Halmashauri hiyo Amos Kanige alisema mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2023/2024 imezingatia dira ya taifa ya maendeleo (2025), sheria ya bajeti namba 11 ya mwaka 2015,mwongozo wa uandaaji mpango wa bajeti 2023/2024uliotolewa na wizara ya fedha mwezi novemba 2022.
Kanige aliongeza kuwa mapendekezo hayo ya bajeti yamezingatia ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi ya mwaka 2020-2025,malengo ya maendeleo endelevu 2030,mpango mkakati wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo 2021/2022-2025/2026 na mapendekezo ya vipaumbele kutoka ngazi za kata,vijiji na maagizo mbalimbali ya viongozi kitaifa.
Hata hivyo Kanige alidai Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 imekisia kukusanya na kupokea jumla ya shilingi 34,111,837,500 kutoka vyanzo vya mapato ya ndani,ruzuku kutoka serikali kuu na kutoka kwa wadau wa maendeleo.
Kanige alifafanua kuwa kutoka katika mapato ya ndani Halmashauri inakisia kukusanya kiasi cha shilingi 2,342,650,000, huku Halmashauri inakisia kupokea ruzuku kutoka serikali kuu kiasi cha shilingi 23,327,988,500 na shilingi 8,441,199,000 fedha kutoka kwa wahisani alifafanua Kanige
Diwani wa kata ya likuyuseka kassim Gunda aliwataka wataalamu kutumia bajeti hiyo inayoandaliwa hivi sasa kuondoa changamoto ya kuwa na makusanyo makubwa tofauti na bajeti iliyowekwa na kulazimika kukubwa na changamoto ya kuhitaji kupanua vifungu katika bajeti .
Baraza la madiwani hilo pia limepitisha mapendekezo ya matumizi ya bajeti hiyo ya shilingi 34,111,837,500 kuwa shilingi 18,758,952,000 zitatumika katika kulipa mishahara ,na shilingi 12,089,035,500 kwa ajili ya miradi ya maendeleo na shilingi 3,263,850,000 zitatumika katika matumizi mengineyo.
Hlmashauri ya wilaya ya Namtumbo kwa mwaka wa fedha 2022/2023iliidhinishiwa kukusanya kiasi cha shilingi 32,485,993,000 ambapo mpaka kufikia desemba 2022 halmashauri hiyo ilikusanya 14,874,648,947.11 na kutumia shilingi 14,199,243,708.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment