January 26, 2023

Kadhi Mkuu wa Dar es Salaam atoa ufafanuzi Majukumu ya Ofisi yake

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

Kadhi Mkuu wa Dar es Salaam Sheikh Ramadhani Kitogo amewataka Waislam nchini kutambua Majukumu ya Ofisi za Makadhi  na kufuata miongozo wanayopewa katika uendeshaji wa mashauri yao.


Ameyasema hayo wakati akiongea na wanahabari ofisini kwake jijini Dar es Salaam na kuwataka Waumini na Waislamu kutambua Majukumu ya ofisi hizo yanaendeshwa kwa kufuata utaratibu.

Amebainisha kuwa suala hilo la uendeshaji limegawanyika katika mafungu matano ya kiuendeshaji ikiwemo Mirathi ya ndoa, Nyumba za wakfu Kutoa maelekezo ya kisheria yahusuyo uislamu sanjari na migogoro ya misikiti.

"Waislam wanahaja ya kubadili mitazamo ya kifikra kutambua ofisi hizi hazishughulikii utoaji wa talaka pekee bila kufuata utaratibu na miongozo iliyowekwa ikiwemo usuluhishi na utoaji wa maamuzi ya mashauri yao"

Amesema kwamba hatua hizo zikifuatwa hakutakuwa na malalamiko Wala manung'uniko Kwani kila Moja ataona haki imetendeka Kwa kujua Baraza linania nzuri ikiwemo vikao kuanzia ngazi ya Kata nyumbani hadi kufikia katika Ofisi hizo.

"Utakuta watu wanashindwa kufuata utaratibu wanatoa lawama za wazi Kwa mihemuko bila kujua Ofisi hizi zinaendeshwa Kwa mujibu wa sheria za dini tujenge hofu ya Mungu twende na utaratibu kuanzia ngazi zilizopo Ili kuwa rahisi Kutoa maamuzi yenye tija Kwa mashauri yao" Amesema Kadhi Kitogo.

Amesisitiza kuwa sio kila shauri linaloletwa ofisini kwake litolewe maamuzi hapo hapo bila kufuata utaratibu kwani huko ni kuwanyima haki stahiki ya kuwasikiliza wengine na kufanya maamuzi ya upande mmoja.

Ameongeza kuwa tuhumu za kwamba ofisi hiyo imekuwa haiwatendei haki wakinamama wanaoleta mashauri sio za kweli kwa mujibu wa uislamu tumekuwa tunaanzia ngazi ya malezi hadi makuzi na uislamu upo wazi kwa miongozo na utoaji haki.

"Haki katika uislamu zimebainishwa wazi katika Quran na Sunah ya Mtume Muhammad S.W.A  kwa mafundisho ya wazi katika sheria za kiislamu hivyo hakuna jipya ila utaratibu wao wa uendeshaji mashauri ni muhimu kufuatwa na wengi watambue utaratibu huo na kuuheshimu"


No comments:

Post a Comment

Pages