HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 19, 2023

RT YATANGAZA TIMU YA TAIFA YA NYIKA MASHINDANO YA DUNIA AUSTRALIA


Kuanzia Kushoto ni, Rais Mstaafu wa RT, Kocha Francis John, Mjumbe wa Kamati ya Riadha Mkoa wa Arusha, Kocha Thomas John , Makamu wa rais RT, William Kallaghe, Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Mbio za Nyika, Kocha Dennis Malle na Katibu Mkuu Mstaafu Wilhelm Gidabuday wakizungumza na Vyombo vya Habari Mbalimbali katika Hoteli ya Premier Palace, Jijini Arusha, Tanzania , Leo 18-01-2023.


Na Mwandishi Wetu


SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT), limetoa Kalenda yake ya matukio ya mwaka 2023 na tayari mikoa wanachama wamekwishatumiwa.


Mikoa inatakiwa izingatie na inatarajiwa kufuatwa na kutekelezwa kikamilifu.


RT inapenda kutoa pongezi za dhati kwa Chama cha Riadha Mkoa wa Arusha (ARAA), kwa utekelezaji wake wa matukio ya Riadha kikamilifu na linaitaka mikoa mingine kuiga mfano wa Arusha.


Mikoa yote, inatakiwa kuhakikisha inafanya vikao na mashindano ya ndani ya mikoa yao na inapaswa kuwasilisha matokeo angalau mwezi mmoja kabla ya tarehe ya mashindano ya Taifa kama ilivyoainishwa kwenye kalenda na hayataahirishwa mwaka huu.


Mkoa ambao hautatekeleza hilo, hawatapewa nafasi kwenye mashindano ya Taifa. 


Shirikisho, halitaki viongozi wa mikoa wanaookota wachezaji ambao hawajawaandaa, wala kuwapima mkoani kwao. 


RT inawakaribisha wadau na wadhamini mbalimbali, kushiriki katika matukio mbalimbali ya riadha, na shirikisho linawakikishia ushirikiano mkubwa na watapata mrejesho kulingana na walichokiwekeza.


VIKAO MBALIMBALI


Katika kupunguza gharama za uendeshaji, Shirikisho kuanzia sasa limejipanga kuendesha baadhi ya vikao vyake vya Kamati Tendaji na Kamati mbalimbali kwa njia ya mtandao 'Virtual meetings'.


WAANDAAJI WA MBIO (RACE ORGANISERS)


RT, inawapongeza waandaaji wote wanaofuata kanuni zilizopo bila usumbufu, wakiongozwa na Kilimanjaro International Marathon, CRDB, NMB, NBC, Mbeya Tulia Marathon na wengineo.


Wale ambao mwaka 2022, wanajijua kuvunja au kutofuata kanuni, Shirikisho halitawafumbia macho na mwaka huu hawatawekwa kwenye kalenda, hadi watoe maelezo na sababu zitakazojitosheleza. 


RT, haiwezi kuwa na matukio yasiyofuata taratibu. Shirikisho limekasimiwa mamlaka ya kusimamia mchezo wa riadha kwa niaba ya serikali, hivyo lina wivu na mamlaka hayo, halitakubali mtu au taasisi yoyote kuliingilia labla iwe kwa maelekezo ya serikali kupitia Wizara au Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

 

MASHINDANO MBALIMBALI
 
Timu ya Taifa ya Mbio za Nyika 'Cross Country', inatarajiwa kuingia kambini Februari Mosi 2023, kambi itakayokuwa ya wiki mbili kujiandaa na maandalizi ya mwisho kuelekea mashindano ya Dunia yatakayofanyika nchini Australia, Aprili 18 mwaka huu.

Timu hiyo iliyopatikana kutokana na mtiririko 'series' zilizofanyika jijini Arusha, inaundwa na Inyasi Sulle, Fabian Nelson, Mathayo Sombi na Josephat Joshua kwa upande wa Senior huku wa akiba no John Nahhay na Herman Sulle, wakati kwa upande wa Junior ni Damian Christian na Kocha ni Denis Malle.

Tanzania itashiriki mashindano ya Vijana U 20 na U 18 Afrika Mashariki nchini Rwanda, Machi 18, 2023.

RT itatumia mashindano hayo kuchagua timu ya Taifa, itakayowakilisha nchi Mashindano ya Afrika U 20 na U 18 Lusaka Zambia Aprili 27 hadi Mei 3.

TEUZI

Kutokana na kukua kwa matumizi ya TEHAMA na upatikanaji wa taarifa mitandaoni, RT imeona iongeze nguvu katika nyanja hiyo na hivyo imemteua Bw. Tullo Stephen Chambo, kuwa Meneja wa Mitandao ya Kijamii (Social Media Manager), ambaye jukumu lake kubwa ni kuhakikisha ubora wa taarifa za Shirikisho kwenye mitandao ya kijamii.
Msemaji wa Shirikisho la Riadha Tanzania, anaendelea kuwa Bi. Lwiza John.

MAREKEBISHO KATIBA

Shirikisho linatarajiwa kukutana na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Januari 20 mwaka huu, kuunda Kamati ya Marekebisho ya Katiba.

Mkutano Mkuu uliopita ambao uliambatana na uchaguzi mdogo Novemba 27, 2022 jijini Dodoma, moja ya ajenda iliyojitokeza ni mapungufu ya katiba na uliazimia yafanyike marekebisho.

Kamati hiyo, itakuwa na kazi ya kupitia katiba na kuainisha mapungufu, Misha kuandaa rasimu itakayotolewa maoni na hatimaye kuwasilishwa Mkutano Mkuu  Mei mwaka huu.

Pia, Kamati hiyo inatarajiwa kupitia kanuni zote za RT na kuangalia mapungufu na kutolea mapendekezo.

No comments:

Post a Comment

Pages