January 06, 2023

 SAKATA LA YANGA SC, FEI TOTO, KIZA KINENE TFF



Na Mwandishi Wetu

SAKATA  la kiungo wa Yanga, Feisal Salum ‘Feitoto’ na klabu ya Yanga bado linaendelea kushika hatamu  katika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania ‘TFF’ chini ya Kamati ya Sheria na hadhi za wachezaji wa soka Tanzania.



Miongoni mwa yaliyojiri siku ya leo katika sakata hilo ni  kusikilizwa kwa pande zote mbili, Yanga  wakimshitaki Feisal kwa kutoonekana kambini huku mchezaji mwenyewe akidai tayari amevunja mkataba na waajiri wake sasa yupo huru.

Katika shitaka hilo, Feisali aliwaasili na Wanasheria wawili ambao pia walisimamia kesi ya Benard Morrison dhidi ya Yanga na kushinda, Makubi Kunju Makubi na Ndurumah Keya Majembe, huku kwa upande wa Yanga wakiwa wanne wakiongozwa na Simon Patrick sambamba na Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Andrew Mtine.


Mahojiano ya kwanza baina ya pande zote tatu (Yanga, Feisal na TFF) yalidumu kwa dakika 40, kuanzia saa 5:15 hadi 5:55 na baada ya hapo walitoka nje kupumzika kama dakika kadhaa  kisha kurudi tena ndani hadi saa 7:00 walipotoka kwaajili ya kupata chakula na wengine kwenda kuswali, shughuli iliyochukua muda wa saa moja na nusu.

Saa 8:50 mchana waliingia tena ndani ya chumba kile wote kila upande kwa kundi lake na kuanza kujadili kwa kina suala hilo, taarifa za ndani kutoka chanzo chetu zimeeleza kuwa walikuwa wakijadili hoja baada ya hoja kutoka upande wa Feisal na Yanga.

Kufikia majira ya  11:10 jioni, wote walikuwa bado ndani ya chumba kimoja wakiendelea na majadiliano, chanzo chetu cha ndani kimeeleza hoja zimekuwa za moto na Kamati bado inazidi kulisikiliza sakata hilo kwa umakini mkubwa. Taarifa zaidi zitakujia hapahapa.


No comments:

Post a Comment

Pages