HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 25, 2023

Serikali yashauriwa kutoa elimu ya usimamizi maliasili

 Na Janeth Jovin

SERIKALI imeombwa kutoa elimu na kuweka usimamizi mzuri wa rasilimali za maliasili ili kuepusha migogoro mbalimbali kwa jamii inayozungukwa na raslimali hizo.


Hayo yalibainishwa hivi karibuni wilayani Bagamoyo mkoani Pwani na Meneja Ufuatiliaji na Tathmini, katika Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, John Noronha wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu uhifadhi wa maliasili yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET).




Noronha amesema ili kukomesha tatizo hilo la migogoro baina ya wananchi na wanyama hasa katika shoroba mbalimbali nchini ni muhimu wananchi wakaelezwa na kupatiwa elimu jinsi rasilimali hizo zitakavyowasaidia kukuza kipato chao.


Amesema wananchi hao wanapaswa kuelimishwa kwa undani umuhimu wa  uhifadhi wa maliasili na jinsi zitakavyo wanufaisha na endapo wakiziharibu wataathirika vipi.


"Ili kuhakikisha sasa rasilimali hizo za maliasili nchini zinaendelea kuimarika na kuleta manufaa kwa Watanzania kupitia shoroba  zilizopo, Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAIDS) kwa kushirikiana na JET tumekuja  na mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili ambao ni wa miaka mitano  na umeanza June 2021, umegharimu  dola za Marekani milioni 30.5.


"Mradi huo unalenga kutatua na kupunguza changamoto zote zinazozikabili hifadhi nchini na kuangalia mapitio ya wanyama  na jinsi ya kuifadhi maliasili endelevu," amesema Noronha.


Noronha amesema utekelezaji wa mradi huo umejikita katika maeneo matatu yakiwa kuzijengea uwezo taasisi  za serikali na binafsi kuhusu uhifadhi wa wanyamapori na kuwapa vifaa mbalimbali vya utendaji.


"Kwa sasa utekelezaji wa mradi huu umeziangalia shoroba saba za hifadhi kati ya 61 zilizopo nchini  ili kuhakikisha zinaleta mafanikio  kwa Watanzania endapo zikisimamiwa vizuri kwa kuepusha migogoro mbalimbali inayosababishwa na shughuli za kibinadamu," amesema


Naye Meneja wa Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi wa Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Dk. Elikana Kalumanga amesema kuwa katika mapitio ya wanyama kuna fursa nyingi zilizopo zikiwemo za kiuchumi, kijamii na kikolojia kutokana na aina mbalimbali za ufugaji zinazoendelea.


Dk. Kalumanga amesema mbali na uwepo wa fursa hizo lakini shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo ni moja ya vitu vinavyoathiri shoroba mbalimbali zilizopo hapa nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John  Chikomo amesema wamekuwa wakitoa mafunzo kwa waandishi wa habari juu ya utunzaji wa mazingira hasa katika masuala ya uhifadhi wa maliasili.


“Mafunzo tuliyoyatoa yamejikita katika utunzaji wa shoroba za wanyamapori kwa lengo la kuisaidia jamii kujua namna ya kutunza na kuhifadhi kwani nyingi zimetoweka kutokana na shughuli za kibinadamu hasa kilimo,”ameeleza.


Naye Mwenyekiti wa JET, Dk. Ellen Otaru amewataka waandishi wa habari kuwa mstari wa mbele kuibua na kuelimisha jamii juu ya athari zitokanazo na shughuli za kibinadamu kama kilimo na nyinginezo ndani ya shoroba pamoja na faida za kiuchumi zinazopatikana.


No comments:

Post a Comment

Pages