January 10, 2023

SOKO LA ASALI LAJA ZANZIBAR

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi  Rahma Kassim Ali amesema kuwepo kwa kituo cha usarifu wa asali  nchini kutaimarisha upatikanaji wa bidhaa hiyo na kuondokana kwa tatizo la kukosekana kwa soko la zao hilo hapa Zanzibar.

Akizungumza katika uzinduzi wa kituo cha kusarifu asali huko Kizimbani Unguja Wilaya ya Magharibi "A"ikiwa ni shamrashamra za kuelekea miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Alisema ujenzi wa kituo hicho utawasaidia wajasiriamali wadogo wadogo kukuza kipato  pamoja na ajira kwa  makundi mbali mbali wakiwemo  vijana na wanawake.

 

 Alisema kua ujenzi wa vituo hivyo ni muhimu kwa upande wa Unguja na Pemba ambapo ni miongoni mwa jitihada za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) katika kuimarisha rasmi Sekta ya Uwekezaji  kiuchumi ili kuleta tija kwa wananchi kwa ujumla.

 

"Vituo hivyo vitasaidia sana kuwawezesha wananchi hasa wanawake kujikwamua kiuchumi na kuondokana kua tegemezi kwani watakua wamejiajiri na kuondokana na ugumu wa  maisha”Alisema  Waziri Rahma.

 

Aidha alisisitiza umuhimu wa kuyatunza majengo hayo kwa watendaji katika kuimarisha usafi ili kuweza kufikia lengo lililokusudiwa, kwani SMZ inamalengo makubwa katika kuwainua wananchi kupitia Sekta ya Uwekezaji Kiuchumi hivyo haitapendeza baada ya muda mfupi majengo hayo kuonekana hayaridhishi kimazingira pamoja utendaji kazi.

Mapema Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Uchumi na Uwekezaji Mudrik Ramadhani Suraga  aliwataka wajasiriamali hao kuzalisha asali iliyo bora ili kuweza kuingia katika ushindani wa kibiashara wa ndani na nje ya nchi kwani SMZ  itaendelea kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia miradi mbali mbali.

 

“Mkizalisha asali bora itaweza kuingia katika soko la ushindani wa kibiashara na Serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyeki wa baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi inamipango mizuri kwa wananchi wake kupitia  sekta hii” Alisema Suraga.

 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Kazi Uchumi na Uwezeshaji wananchi kiuchumi  Maryam Abdalla Juma alisema ujenzi wa kituo hicho ulianza mwaka jana mwezi Machi,2022 na umegharimu jumla zaidi ya shilingi  Milioni mia mbili (236,325,000/= ).

 

Alifahamisha kwamba katika juhudi ya kuwawezesha wananchi kiuchumi jumla ya wajasiriamali 753 kutoka Uguja na Pemba wakiwemo wanaume 280 na wanawake 473 walipatiwa mafunzo ya ufugaji wa nyuki kwa nadharia na vitendo ikiwa ni hatua ya kuwajengea uwezo katika utaalam wa kufuga nyuki.

 

Aidha Katibu Mkuu huyo  alisema kua ununuzi wa vifaa vya ufugaji wa nyuki kwa wajasiriamali umegharimu jumla ya shilingi milioni mia sita nukta 2.5 (625,000,000/=) ambapo vifaa hivyo tayari vimeshagaaiwa kwa wajasiriamali wote waliopatiwa mafunzo Unguja na Pemba kupitia Ofisi za Mikoa.

 

Naye mjasiriamali wa ufugaji wa asali faraja Ali Hassan ameishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na Wizara ya Kazi, Uchumi na Uwekezaji  kwa kuwapatia mafunzo hayo pamoja na kuwajengea kituo cha kusarifu asali hatua itakayowasaidia katika kujikwamua na hali ngumu ya maisha hivyo aliahidi kuyaafanyia kazi mafunzo waliyopatiwa kwa vitendo.

No comments:

Post a Comment

Pages