January 10, 2023

Wananchi Pemba wajitolea Ardhi kwa ajili ya Ujenzi wa Kituo cha Afya

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Zanzibar, Rahma Kasimu Ali amewashukuru wananchi wa Kijiji cha Gando Pemba kwa uzalendo wao wa kutoa eneo la ardhi kwa kikosi cha KMKM kwa ajili ya ujenzi wa  kituo cha Afya.

Kauli hiyo ameitowa wakati alipoweka jiwe la msingi katika eneo hilo ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar kutimiza miaka 59 tangu yalipotokea Mwaka 1964.

Alisema wananchi wa Kijiji cha Gando wameonesha  moyo wa uzalendo na kueka kando itikadi za kisiasa kwa kutoa eneo lao kuwapa Kikosi cha KMKM kujenga Kituo cha Afya hivyo ni jambo  jema na la kuwashukuru.

“Hakika nyinyi ni wana mapinduzi halisi na mmeonesha kwa vitendo jinsi mnavyoshirikiana na Serikali kuleta maendeleo katika eneo lenu. Nasaha zangu kwa wananchi wengine Unguja na Pemba kuiga  mfano wenu hasa ikizingatiwa kuwa maendeleo hayana chama, nakushukuruni kwa dhani kwa kutoa eneo lenu kwajili ya kituo cha afya”

Pia aliwashukuru mafundi na vibarua wa KMKM, kwa hatua waliyofikia katika mradi wa ujenzi kituo hicho kwa kwenda muda na kwa gharama ndogo kwani  bila ya hivyo gharama zingelikuwa kubwa zaidi kwa Serikali katika kutekeleza mradi huo.

Hivyo waziri Rahma alimuagiza Komodoo wa KMKM Azana Hassan Msingiri kuwatizama kwa jicho la huruma mafundi na vibarua waliyofanikisha ujenzi huo ili kuthamini jasho na uzalendo wao.

Alieleza kwamba anaamini mradi huo wa kituo cha afya utakapo kamilika huduma bora zitapatikana kwa askari pamoja na wananchi kama vile ambavyo zinaonekana kwenye Hospital ya KMKM Kibweni Unguja.


Aidha alisisitiza umuhimu wa kuwepo vifaa, madaktari, manesi na maodali wa kutosha kwa mujibu wa mwongozo wa vituo vya afya uliotayarishwa na Wizara ya Afya Zanzibar katika kituo hicho kitakapoanza kutoa huduma.

 Vile vile aliwakumbusha wafikirie umuhimu wa  kutoa huduma za mama na mtoto ili wananchi  wa Gando pamoja na vitongoji vyake wasipate tabu na usumbufu wa kwenda kujifungulia maeneo ya mbali jambo ambalo litakuwa sio sahihi.

Aidha alisema hatua ya wananchi kutoa eneo lao inaonesha taswira kwamba wananchi hao wako tayari kushirikiana na KMKM kutoa taarifa za watu wanaotaka kusafirisha magendo ya karafuu na magendo mengine ikiwemo uvuvi haramu na uchafuzi wa bahari hali ambayo itasaidia kuimarika kwa kambi ya KMKM Gando.

“ kuimarika kwa kambi hiyo kusaidia Serikali na jamii juu ya uvuvi haramu na uhifadhi wa bahari yetu. Hivyo basi, ushauri wangu kwenu wanaKMKM mzidishe mashirikiano na wananchi wa Kijiji cha Gando na vijiji jirani kwani kufanya hivyo kutasaidia sana ufanisi wa kazi zenu nzito ambapo huwa mnakabiliana na watu ambao hamuwaoni lakini kwa msaada wa wananchi basi mtawaona”Alisema waziri huyo.

Sambamba na hayo Waziri Rahama alimuagiza Katibu Mtendaji wa kamisheni ya ardhi Zanzibar kuwapatia  hatimiliki ya eneo hilo ambapo ombi  hilo liliwasilishwa kwa waziri wa ardhi kupitia  risala iliyosomwa awali.

 

 

 

No comments:

Post a Comment

Pages