January 10, 2023

Viongozi wa Vyama vya Upinzani Wampongeza Rais Samia kuruhusu Mikutano ya Hadhara

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam


 Baada ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kutangaza kuruhusu kufanyika kwa mikutano ya hadhara ya kisiasa nchini,Vyama mbalimbali vya siasa vimejitokeza na kupongeza hatua hiyo.
Wakizungumza na waandishi jijini Dar es salaam viongozi wakuu wa vyama hivyo wamesema hatua hiyo ya Rais Dkt. Samia ni ya kupongezwa na ni muhimu kwa maslahi mapana ya Taifa.

Akizungumza katika mkutano huo,Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi Cuf, Profesa Ibrahim Lipumba amesema kuwa kauli ya Rais Samia imeleta matumaini makubwa kwa siasa za Tanzania na imeonyesha ni jinsi gani ana maono ya kukuza mashirikiano nchini.

Nae, Mwenyekiti wa Chama cha ADC,Hamad Rashid amesema kuwa tukio hilo  kwa viongozi wa vyama vya siasa ni la kihistoria na limeleta fursa kwa wananchi sasa kuweza kusikiliza sera za vyama vya siasa na kuchagua viongozi wao ambao wameridhishwa na sera zao.

Ameongeza kuwa Rais Dkt Samia ametembea katika kiapo chake na anafaa kuungwa mkono na kila mwenye kutambua thamani ya demokrasia.

Hata hivyo Hamad Rashidi amewataka wanasiasa kutumia fursa hiyo kwa kuzingatia sheria na bila kuleta uvunjifu wa amani.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa amesema kuna kila sababu ya kumpongeza Rais Dkt Samia kwa kuonyesha uzalendo mkubwa kwa kuzungumza na vyama vyote kikiwemo Chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema)kupitia mwenyekiti wao,Freeman Mbowe.

"Hii ndiyo Tanzania tunayoitaka,tukae pamoja,tubishane pamoja na Hii ni sababu kubwa ya kumpongeza Rais na baraza la vyama vya siasa litampa ushirikiano mkubwa na kumuunga mkono bila kuangalia itikadi za vyama vyao"alisema.

Nae, Joseph Selasini wa Chama cha NCCR Mageuzi amesema maamuzi ya jana ni maamuzi mazito sana kufanywa na Rais ambaye naye chama chake kiko kwenye ushindani kisiasa hivyo ni ya kuungwa mkono.

Ameongeza kuwa sasa wanasiasa watamsaidia Rais kwa kuwasema na kuwakemea wote wanaolihujumu Taifa wakiwemo wala rushwa.


No comments:

Post a Comment

Pages