*Awataka watengeneze utaratibu wa waisaidia Namungo ifanye vizuri zaidi
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wafanyabiashara mbalimbali wilayani Ruangwa, Lindi watengeze utaratibu wa kuiwezesha timu ya mpira wa miguu ya Namungo ili iweze kufanya vizuri zaidi katika michuano ya ligi kuu inayoendelea.
Alitoa wito huo jana jioni (Jumamosi, Desemba 31, 2022) baada ya kuzindua tawi la wakereketwa wa timu ya Namungo lililopo katika mtaa wa Kongo wilayani Ruangwa. Namungo kwa sasa inashikilia nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi kuu ya NBC.
“Namungo imeendelea kufanya vizuri, sasa katika msimamo wa ligi ipo namba tano. Lazima tujenge utamaduni wa kujitoa na kusimamia jambo letu, ufunguzi wa tawi hili ni muendelezo wa kusukuma mbele maendeleo ya timu yetu. Lazima tujipange vizuri.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema amefurahi kuona wana-Ruangwa wanatambua umuhimu wa timu ya Namungo yenye mchango mkubwa katika kuchangia maendeleo ya wilaya yao kiuchumi. “Tushirikiane kuhakikisha Namungo ienaedelea kubaki ligi kuu.”
Kwa upande wake, Katibu wa Tawi hilo lenye wanachama 103, Pendo Sungura alisema lengo la umoja huo ni kuhakikisha wanashirikiana na wadau wengine katika matawi mengine kwa ajili ya kuiwezesha timu yao ifanye vizuri zaidi.
No comments:
Post a Comment