HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 19, 2023

KILUPI - AONYESHA NIA YA KUISAIDIA SKULI YA BUBUBU ZANZIBAR

KATIBU wa Idara ya Organazesheni ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar,Omar Ibrahim Kilupi akitoa mkono wa pole wa sh.200,000 kwa familia ya Ali Makame Ali ambayo nyumba yao iliunguliwa na moto katika kijiji cha Kama.

 

NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR

 

KATIBU wa Idara ya Organazesheni ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)Zanzibar, Omar Ibrahim Kilupi,amesema ataendelea kusaidia uongozi wa shule ya Sekondari ya Bububu kama sehemu ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ilivyoelekeza.

 

Kauli hiyo ameitoa jana wakati akikabidhi matofali 1,000 kwa uongozi wa shule ya Sekondari ya Bububu kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa shule hiyo.

 

Alisema akiwa kama kiongozi wa CCM ana imani kuwa elimu ndio msingi wa maisha kwa vijana ambao baadaye watakuja kuwa viongozi mbalimbali.

 

"Ninachoomba wazazi wa wanafunzi pamoja na viongozi wenzangu tuhakikishe tunakuwa bega kwa bega kuhakikisha wanafunzi hawa tunawasaidia kwa hali na mali,"alisema..

 

Katika maelezo yake Katibu huyo alisema hivi karibuni kumetokea mabadiliko makubwa ya ufaulu wa wanafunzi katika shule hiyo kwenye mitihani ya taifa ambapo alama ya daraja zero zimepungua kwa kiasi kikubwa huku kwa upande wa  daraja la pili imeongezeka. "Nakumbuka mwaka uliopita nilileta chakula cha thamani ya sh.600000 kwa ajili ya wanafunzi ambao wameweka kambi ya kujisomea maandalizi ya mitihani ya taifa na tumeanza kuona faida kubwa katika mabadiliko haya hivyo nitaendelea kusaidia shule hii,"alisema.

 

Wakati huo huo Katibu huyo wa Idara ya Organazesheni Kilupi aliongoza harambee ya kuchangia familia ya Ali Makame Ali ambayo nyumba yao iliunguliwa na moto katika kijiji cha Kama.

"CCM imeguswa na tukio hili la kuunguliwa na moto na mimi binafsi.

 
ninatoa sh.200,000 lakini nachoomba wenzangu wachangie chochote kwa ajili ya kuwafariji familia hii,"alisema.

 

Kwa upande wake Katibu wa CCM,wilaya ya Mfenesini, Mwasiti Hassan Mohamed alisema katika mambo ambayo yameelekezwa na chama ni utekelezaji wa ilani na kwamba kitendo hicho cha kuleta matofali kwa uongozi wa shule hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya chama katika elimu.

 

"Sisi tulikuja hapa wakati wa sherehe za Jumuiya ya Umoja wa Wazazi na jambo ambalo uongozi wa shule ulisema kuwa eneo hili ni hatarishi kwa wanafunzi na waliomba sana matofali kwa ajili ya kujenga ukuta,"alisema.

 

Alisema kitendo cha Katibu huyo wa Idara ya Organazesheni kutoa matofali hayo uongozi wa CCM wa wilaya ya Mfenesini imefurahishwa sana katika utekelezaji huo.

 

Naye Mwenyekiti wa kamati ya Shule ya Sekondari ya Bububu Machano Mohamed Juma alisema matofali hayo 1000 yaliyotolewa na Katibu wa Idara ya Organazesheni ni msaada mkubwa.

 

"Pamoja na kwamba bado tunahitaji zaidi lakini tulichopewa
kitatufikisha mbali bado tunawaomba viongozi wengine waje kutoa msaada kwa ajili ya kukamilisha jambo hili,"alisema

 

No comments:

Post a Comment

Pages