March 21, 2023

Mikoa 18 kupata mvua kubwa

 

 Na Irene Mark


TAHADHARI ya mvua kubwa imetolewa kwa mikoa 18 hapa nchini huku wakazi wa maeno hayo wakitakiwa kuchukua hatua za kuzuia athari zitakazosababishwa na mvua hiyo.

Mikoa itakayopata mvua kubwa kuanzia leo Machi 21,2023 ni Mara, Simiyu, Mwanza, Shinyanga, Dodoma, Singida, Arusha, Manyara, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe, Rukwa, Dar es Salaam, Pwani (ikihusisha visiwa vya Mafia), Lindi, Mtwara, visiwa vya Unguja na Pemba.



Tahadhari hiyo ya siku tano imetolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kipindi hiki ambacho msimu wa masika umeanza kwa mujibu wa utabiri wa msimu uliotolewa Februari 22,2023 na Kaimu Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Dk. Ladislaus Chang’a.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya siku tano mvua pia inatarajiwa kwenye baadhi ya maeneo ya mikoa ya Lindi na Mtwara kesho Jumatano Machi 22,2023  itakayopata mvua kubwa.

Machi 23,2023 pia TMA imeeleza kwamba “Angalizo la mvua kubwa limetolewa kwa maeneo mengi ya mikoa ya Dar es Salaam, Pwani (ikihusisha visiwa vya Mafia) pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Pamoja na tahadhari hiyo, TMA imezitaka mamlaka zinazohusika na maafa wakishirikiana na wakazi wa maeneo hayo kuchukua hatua za kudhibiti athari zinazoweza kujitokeza ikiwemo makazi ya wananchi kujaa maji.

Mamlaka hiyo pia imetoa angalizo la mvua kubwa kwa mikoa ya Lindi na Mtwara kwa siku ya Ijumaa Machi 24,2023 hivyo hatua za tahadhari zichukuliwe kudhibiti athari zinazoweza kujitokeza.

Athari zinazoweza kujitokeza ni baadhi ya makazi kujaa maji na kuathirika kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi.

No comments:

Post a Comment

Pages