March 22, 2023

NMB yatenga mikopo ya bilioni 20 Sekta ya Kilimo

Benki ya NMB imetenga mikopo ya shilingi bilioni 20 itakayotumika kuchangia maendeleo ya sekta ya kilimo nchini ikiwa ni dhamira ya benki hiyo katika kuinua ufanisi wa sekta hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kushuhudia uzinduzi wa programu ya Serikali ya vijana maarufu kama ‘Building Better Tomorrow’ (BBT) Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma linalolenga kukuongeza ushiriki wa vijana wa Kitanzania katika kilimo biashara, Mkuu wa Wateja Wadogo wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi alisema juhudi za benki zinalenga kuunga mkono Ajenda ya 10/30 ya Serikali huku akibainisha kuwa jitihada za benki yake siyo to zitasaidia katika kupanua shughuli za kiuchumi katika sekta ya kilimo bali pia zitasaidia kuongeza usalama wa chakula.



“Benki ya NMB ni mdau mkubwa sana wa serikali na tumekuwa tukishirikiana na sekta mbalimbali ikiwemo sekta hii ya Kilimo. Sekta hii ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu, Benki yetu itaendelea kuwa bega kwa bega na wizara ya kilimo ili kuhakikisha maono yake katika sekta ya Kilimo hapa nchini yanatimia na kuzidi kukuza uchumi wa nchi yetu. Ni imani yetu kuwa juhudi zetu zitasaidia kujenga sekta ya kilimo imara yenye ushindani na jumuishi na yenye sifa ya kuimarika kwa ufanisi, utofauti na yenye kuongeza mapato,” Mponzi alisema.



Mponzi alisema mara baada ya benki yake kushirikishwa na Wizara ya kilimo juu ya mpango huo wa Building a Better Tomorrow, benki yake haikusita kuridhia kushirikiana na wizara na ilitoa wataalamu wake kudadavua vyema mkakati huo na badae kuanzisha huduma ambazo zitasaidia ufanisi wa mkakati huu.


“Tumekuja na bidhaa ya mkopo maalum wenye riba rafiki ambao utawawezesha Vijana kupata mitaji ya kuanzisha au kuendeleza biashara za kilimo, ufugaji na uvujiwa. Maana tunatambua Changamoto kubwa ya Vijana wengi kuingia katika kilimo ni ukosefu wa mitaji, hivyo Benki ya NMB imeona kwa kuanzisha mkopo huu maalum basi wengi watashawishika na adhma ya Building a Better Tomorrow itatimia,” alisema Mponzi.

Aliwataka vijana kuchangamkia fursa hiyo kwa kutembelea matawi ya benki hiyo yaliyopo nchini kote huku akisema kuwa benki yake imetoa mafunzo ya kifedha kwa vijana zaidi ya 800 ambao wamechaguliwa kushiriki program ya BBT.



Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe wakati wa uzinduzi wa programu ya BBT alisema tayari wizara yake imeshirikisha benki mbalimbali zinazofanya kazi nchini Tanzania kuanzisha fungo maalum yaani ‘matching fund’ ili kuunga mkono juhudi za wizara hiyo zinazolenga kufufua na kufungua sekta ya kilimo.



“Nina furaha kutangaza kwamba tayari nimeshapokea barua kutoka benki ya NMB na wametoa ahadi ya kutoa shilingi bilioni 20 ambazo zimetengwa na benki hiyo kusaidia mpango huu na tutaendelea kushirikiana na benki hiyo katika kutekeleza hili,” Bashe alisema.

Bashe alisema Serikali imejipanga kikamilifu kusaidia vijana katika mnyororo wa thamani wa sekta ya kilimo ili kuwasaidia kutimiza ndoto zao kikamilifu kupitia biashara ya kilimo.



Kuhusu dhamira ya Serikali ya kuongeza thamani ya korosho ya Tanzania, Bashe alibainisha kuwa kuanzia bajeti ya mwaka wa fedha wa 2026/2027, korosho za haitauzwa kama mali ghafi.

Lengo la serikali ni kufikia ukuaji wa zaidi ya asilimia 10 kwa sekta ya kilimo ifikapo 2030.

No comments:

Post a Comment

Pages